Majina ya wapenzi wa jinsia moja kutotangazwa hadharani Tanzania

Mapenzi ya jinsia moja ni haramu Afrika Mashariki na adhabu yake ni hadi miaka 30 jela.
Maelezo ya picha,

Mapenzi ya jinsia moja ni haramu Afrika Mashariki na adhabu yake ni hadi miaka 30 jela.

Serikali ya Tanzania haiwezi kuchapisha majina ya watu wanaoshukiwa kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja.

Daktari Hamisi Kigwangalla, ambaye ni naibu waziri wa afya, ndiye amekuwa akisema kuwa majina hayo yangechapishwa, akisema kuwa wale wanaojitangaza mitandaoni kuwa wapenzi wa jinsi moja watakamatwa.

"Tulifuta mkutano wa waandishi habari. Hatutatangaza majina ya wale wanaojitangaza mitandaoni kwa sababu za kiufundi." aliandika kwenye mtandao wa Twitter.

Saa tatu baadaye alithibitisha kwa wafuasi wake kwenye Twitter kuwa, majina hayo yapo na utawala ulikuwa na lengo la kuyaweka hadharani.

Kisha baadaye tena akaandika kuwa ili kuzuia watu kuficha ushahidi, mbinu zao zimebadilika na umma utajulishwa jinsi wizara ya afya itaendesha zoezi hilo.

Mapenzi ya jinsia moja ni haramu Afrika Mashariki na adhabu yake ni hadi miaka 30 jela.