Uganda yaongoza kwa ufasaha wa lugha ya kiingereza Afrika

Uganda imetajwa kuwa nchi yenye raia wanaozungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha barani Afrika.

Utafiti uliofanywa na shirika la lugha duniani World Linguistic Society umesema Uganda inaongoza ikifuatiwa na Zambia halafu Afrika Kusini ikiwa katika nafasi ya tatu na Kenya katika nafasi nne.

Maelezo ya picha,

Uganda imetajwa kuwa nchi yenye raia wanaozungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha zaidi barani Afrika

Kulingana na gazeti la The New Vison nchini Uganda, utafiti huo unajiri kufuatia kanda ya video iliomuonyesha malkia wa urembo kutoka Rwanda akishindwa kujielezea kiingereza.

The New Vison linasema kuwa mwaka 2015, mmoja wa malkia hao wa Urembo katika shindano la Malkia wa urembo nchini Rwanda Uwase Honorine alishindwa kujibu maswali aliyoulizwa na majaji wa shindano hilo.

Rwanda iliokuwa chini ya koloni ya Ufaransa ilianza kuzungumza Kiingereza baada ya kukosana na Ufaransa.

Gazeti la The New Vision linasema kuwa kiingereza nchini Uganda ndio lugha rasmi, na ndio lugha inayotumiwa katika shule na taasisi tofauti nchini humo.

Watoto huanza kujifunza lugha hiyo katika shule za msingi.

The New Vison linasema kuwa hivi majuzi serikali iliziagiza shule kufunza lugha za nyumbani kwa wale wanaosoma katika shule za msingi lakini ikasisitizia kuwa Kiingereza ndio lugha itakayotumiwa katika mtaala.

Mataifa yanayozungumza kiingereza kwa ufasaha:

1.Uganda

2. Zambia

3. South Africa

4 . Kenya

5. Zimbabwe

6. Malawi

7. Ghana

8. Botswana

9. Sudan