Kambi za Tanzania zakumbwa na msongamano wa wakimbizi

Kati ya watu 600 na 1000 huwasili kwenye kambi za Tanzania kila siku Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kati ya watu 600 na 1000 huwasili kwenye kambi za Tanzania kila siku

Tatizo la kiafya huenda likakumba kambi za wakimbizi nchini Tanzania, kufuatia kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaowasili nchini humo, kwa mujibu wa shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka MSF.

Wakimbizi 290,000 ambao robo tatu yao hutokea nchini Burundi, wamejazana kwenye kambi tatu za Nyarugusu, Mtendeli na Nduta.

Kambi ya Nduta iliyobuniwa ili kupunguza msongamano kwenye kambi ya Nyarugusu iliyo mkoa wa magharibi wa Kigoma ina watu 117,000 ambao ni mara mbili zaidi ya idadi inayoweza kuhifadhiwa.

Kambi hiyo inatarajiwa kuwapokea watu 150,000 ifikiapo mwezi Aprili ikiwa watu kati ya 600 na 1000 wanaowasili kila siku wataendelea kuingia.

MSF ambayo inatoa huduma za afya katika kambi hiyo, inasema kuwa imeandikisha nyongeza ya watu wanaotafuta matibabu.

Mkuu wa MSF David Nash, anasema kuwa kuna hitaji la dharura la kujenga kambi nyingine.