Uavyaji mimba: Wachangisha fedha kupinga sheria ya Trump

Donald Trump akipinga sheria ya kuruhusu uavyaji mimba Haki miliki ya picha AFP
Image caption Donald Trump akipinga sheria ya kuruhusu uavyaji mimba

Kongamano la kuchangisha fedha linafanyika nchini Ubelgiji baadae leo ili kuimarisha afya ya uzazi miongoni mwa wanawake katika mataifa masikini ambayo yameathirika kufuatia hatua ya Marekani kutishia kusimamisha msaada kwa serikali zinazokubali uavyaji mimba kama njia ya mpango wa uzazi.

Siyo mara ya kwanza kwa utawala wa Republican kusimamisha ufadhili kwa huduma za mpango wa uzazi katika mataifa masikini yanayokubali uaviaji mimba.

Hata hivyo utawala wa sasa wa Rais Donald Trump umeweka vikwazo zaidi na kulenga mashirika yasiyo ya serikali ambayo hutoa ushauri nasaha kuhusu uavyaji mimba.

Hii ina maana kwamba huenda ufadhili ukasimamishwa kwa mashirika yanayowasaidia wagonjwa wa ukimwi pamoja na huduma za afya ya uzazi.

Ili kujaza pengo hilo mataifa ya Uholanzi, Sweden, na Denmark yameandaa kongamano maalum la kuchangisha fedha mjini Brussels, Ubeljiji.

Hazina hii inajulikana kama 'Haki ya mwanamke kuamua'.

Baadhi ya wadadisi wamesema licha ya juhudi hio, hata hivyo kunahitajika mamilioni ya dola ili kuboresha afya ya uzazi miongoni mwa wanawake.