Muuguzi afariki baada ya wauguzi kuogopa kumgusa

Salome Karwah amewacha watoto wanne Haki miliki ya picha Time Magazine
Image caption Salome Karwah amewacha watoto wanne

Muuguzi raia wa Liberia Salome Karwah ni baadhi ya wale waliotajwa na jarida la Time magazine kuwa mtu bora wa mwaka, mwaka 2014 baada ya kushiriki katika vita dhidi ya ugonjwa wa Ebola

Alifariki mjini Monrovia wiki iliyopita baada ya kujifungua mtoto wa kiume.

Mumewe aliambia BBC kuwa wauguzi walikuwa na hofu ya kumgusa kwa kuwa walihofia kuambukizwa ugonjwa wa Ebola, licha ya kupatikana kutokuwa na ugonjwa huo hivi majuzi.

Hospitali alimokuwa haijasema lolote na maafisa wanasema kuwa wanachunguza kifo chake.

James Harris alisema kuwa mkewe alikuwa amejifungua mto wao wa nne kwa njia ya upasuaji tarehe 17 mwezi Februari lakini alirudishwa hospitalini baada ya kukumbwa na matatizo.

"Walilazimika kungoja ndani ya gari kwa saa tatu, kwa sababu wauguzi walikuwa na hofu ya kumgusa," bwana Harris alisema.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kisa cha Salome kinaashiria unyanyapaa unaowakumba walionusurika kutokana kwa ugonjwa huo

"Nilienda mimi mwenyewe kwenye chumba cha dharura nikachukua kiti cha magurudumu na kumpeleka mke wangu kwenye chumba cha upasuaji."

"Kilichoniumiza zaidi ni kuwa muuguzi ambaye alikuwa kwenye zamu alikuwa Facebook," alisema Harris.

Anaamini kuwa wahudumu wa afya hawakuchukua hatu za dharura, kwa sababu alikuwa amenusurika kutoka kwa Ebola na labda walifikiri kuwa bado alikuwa na ugonjwa huo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Watu waliotaja na Time Magazine kuwa bora mwaka 2014