Waliokanganya tuzo za Oscars sasa wapewa ulinzi

Mahasibu waliokanganya mashabiziki wa tuzo za Oscars Brian Cullinan na Martha Ruzi
Image caption Mahasibu waliokanganya mashabiziki wa tuzo za Oscars Brian Cullinan na Martha Ruzi

Mahasibu wawili waliokanganya watu katika tuzo za Oscars sasa wamepewa walinzi kufuatia ripoti kwamba wamepokea vitisho vya kuuawa katika mitandao ya kijamii.

Kampuni ya mahasibu ya PriceWatersHouseCoopers PwC imesema kuwa wawili hao wamepewa ulinzi katika makaazi yao.

Mtandao wa watu maarufu TMZ.com umesema kuwa ulinzi umewekwa katika makao ya Brian Cullinan na Martha Ruzi kufuatia makosa yao katika tuzo hizo.

TMZ.com inasema kuwa wawili hao wanahofia maisha yao.

makosa hayo yalipelekea filamu ya muziki ya La La Land kupewa tuzo ya picha bora kwa muda badala ya Moonlight.

Siku ya Jumatano, ilibainika kuwa hawatepewa tena kandarasi ya kushiriki tena katika tuzo hizo.

Lakini TMZ.com imesema kuwa hawatafutwa kazi yao ya uhasibu.

Msemaji wa PWC Carey Bodenheimer alisema kuwa wamepewa ulinzi baada ya anuani na picha ya familia zao kuchapishwa mitandaoni.