Rais Magufuli aamrisha kutwaliwa pasipoti ya mwanakandarasi

Rais Magufuli aamrishwa kutwaliwa kwa pasipoti ya mwanakandarasi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Magufuli aamrishwa kutwaliwa kwa pasipoti ya mwanakandarasi

Rais wa Tanzania John Magufuli ameamrisha kutwaliwa kwa pasipoti ya mwanakandarasi wa India, ambaye ameshindwa kumaliza mradi wa maji kwa wakati ufaao.

Mwanakandarasi huyo Rajendra Kumar, wa kampuni ya Alliance Private Limited, alistahili kukamilisha mradi huo mwezi Machi mwaka 2015.

Lakini kulingana na waziri wa maji, alishindwa kufanya hivyo baada ya kuishiwa na pesa.

Mradi huo unaogharimu dola milioni 12.2, ni wa kuchimba visima 10 kwa manufaa ya watu 82,000 eneo la kusini mashariki mwa nchi la Lindi.

Serikali inafadhili mradi huo kwa mkopo kutoka kwa Muungano wa Ulaya na Benki ya Maendeleo ya Uerumani.

"Hatuwezi kuruhusu watu wa Lindi kuendelea kukumbwa na uhaba wa maji. Mradi huu umechelewa kwa miaka miwili kwa sababu mwanakandarasi ameamua kupeleka pesa India," alisema Rais Magufuli.

Pia aliwalaumu maafisa wa wizara ya maji kwa kuwa asilimia 90 ya pesa hizo tayari zimetumika na mradi uko mbali na kukamilishwa.