Serikali na familia watofautiana juu ya mazishi ya Tshisekedi DR Congo

Marehemu Etienne Tshisekedi
Image caption Marehemu Etienne Tshisekedi

Mwili wa kiongozi wa upinzani nchini DR Congo Etienne Tshisekedi hautarudishwa nyumbani wiki hii kama ilivyopangwa.

Familia ya Bwana Tshisekedi aliyefariki mwezi uliopita nchini Ubelgiji akiwa na umri wa miaka 84 alikuwa amepanga kufanya mazishi nchini DR Congo Jumamosi inayokuja.

Nduguye mdogo bwana Tshisekedi Gerard Mulumba aliambia BBC kwamba familia haijakukubaliana na serikali kuhusiana na eneo atakalozikwa marehemu mjini Kinshasa.

Familia ya Tshisekedi wanataka mwili uzikwe katika makao makuu ya chama cha UPDS alichanzisha.

Lakini serikali inataka kumzika katika maziko ya Gombe yalioko katikati ya mji.

Hakujakuwa na jibu rasmi kuhusiana na tangazo hilo.

Kifo cha Bwana Tshisekedi kimeliweka taifa hilo katika hali tete kwa kuwa kilijiri wakati ambapo kulikuwa na majadiliano kati ya serikali na upinzani kumaliza mgogoro wa kisiasa ambao umesababishwa na hatua ya rais Kabila kukataa kujizulu baada ya kukamilika kwa muhula wake wa kuongoza mnamo mwezi Disemba.

Uchaguzi unakaribia kabla ya mwisho wa mwaka na mwana wa Tshisekedi Felix amechaguliwa kuongoza upinzani katika mazungumzo hayo..