Marekani yapeleka mfumo wa kujilinda na makombora K.Kusini

Mfumo wa ulinzi wa THAAD
Maelezo ya picha,

Mfum huo unaowekwa kwenye maeneio ya miinuko (THAAD) ukizinduliwa kukabiliana na majaribio ya makombora

Jeshi la Marekani linasema kuwa limeanza kupeleka mfumo tata wa kijilinda dhidi ya makombora ya masafa nchini Korea Kusini.

Mfumo huo wa ulinzi unaowekwa kwenye maeneo ya miinuko unaofahamika kama-Thaad- kwa kifupi umetengenezwa kwa ajili ya kujilinda dhidi ya vitisho vya Korea Kaskazini.

Hatua ya kuweka mifumo hiyo imechukuliwa siku moja baada ya Korea Kaskazini kufyatua makombora ya masafa ya kadri, na hivyo kuvunja vikwazo vya kimataifa.

Lakini mipango ya Marekani ya kupeleka mfumo huo wa ulinzi katika Korea Kusini imewaudhi wengi nchini Korea Kaskazini na Korea Kusini pamoja na mataifa jirani katika kanda hiyo.

Shirika la habari la Korea Kusini Yonhap limesema kuwa harakati za kujenga mfumo wa Thaad zilianza Jumatatu, huku baadhi ya mitambo ya mfumo huo ikisafirishwa kwa ndege kutoka Marekani hadi kwenye kituo cha kijeshi cha anga kilichopo karibu na mji mkuu Seoul.

Korea Kusini imesema kuwa mfumo huo utaanza kufanya kazi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Rais wa Marekani Donald Trump ameapa kumaliza mipango ya Korea Kaskazini ya kujenga na kuzindua makombora yenye uwezo wa kufika Marekani, akisema kuwa kuanzia Januari mwisho ''hilo halitatokea''.

Namna mfumo wa kujilinda na makombora wa DHAAD unavyofanya kazi

Maelezo ya picha,

Namna mfumo wa ulinzi wa THAAD unavyofanya kazi

Wengi miongoni mwa raia wa Korea Kusini wanaamini kuwa mfumo wa ulinzi wa Marekani utalengwa na mashambulio, na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wanaoishi karibu na vituo vya kijeshi, na wapinzani wa mfumo huo wamekuwa wakifanya maandamano kuupinga.

Mwezi Agosti mwaka jana, wakazi wa jimbo la kusini mashariki la Seongju walionyesha upinzani dhidi ya mfumo wa Thaad kwa kunyoa nywele zote vichwa vyao.

Uchina Inapinga vikali kupelekwa kwa mfumo huo. Mwandishi wa BBC Stephen Evans aliepo mjini Seoul ameelezea hofu ya waChina kwamba mfumo huo unaweza kuingia ndani ya eneo la Uchina, suala ambalo linaweza kuondoa uwiano wa nguvu za kujilinda uliopo katika kanda hiyo.

Pia kumekuwa na hasira miongoni mwa wanunuzi kiChina dhidi ya Kiwanda cha Korea Kusini cha Lotte, kwa kuruhusu mfumo wa Thaad kuwekwa kwenye moja ya maeneo yake.