Ujumbe wa dhihaka wamsaidia polisi kutibiwa unene India

DK. Muffazal Lakdawala, kulia ,pamoja na Inspekta Daulatram Jogawat Haki miliki ya picha SAIFEE HOSPITAL
Image caption DK. Muffazal Lakdawala, kulia ,alimtibu Inspekta Daulatram Jogawat

Taarifa ya Twitter iliyotumwa na mwandishi maarufu wa India kumuaibisha polisi mmoja wa nchi hiyo kwa kuwa mnene kupindukia imekuwa na matokeo ambayo hayakutarajiwa- Kupata huduma bure ya upasuaji wa kupunguza uzito mjini Mumbai.

Mwandishi alituma ujumbe wa Twitter wa picha ya Bwana Jogawat mwezi uliopita, akisema kuwa polisi huyo aliyeko Mumbai alikuwa na mpango wa "kuweka usalama mzito" kwa ajili ya uchaguzi wa mitaa. Ujumbe huo uliosambazwa sana uliifanya hospitali ya Saifee kujitolea kulipia gharama za matibabu ya upasuaji wake.

Hospitali hiyo ilisema kuwa Inspekta Jogawat anaendelea vyema baada ya upasuaji, na uzito wa mwili wake unaweza kupungua hadi karibu kilo 80 mwaka ujao. Alikuwa na uzito wa kilo 180 kabla ya upasuaji.

Upasuaji huo kwa lugha ya kitaalam -Bariatric surgery, hutumiwa kama tiba ya mwisho kwa mtu mwenye unene wa kupindukia unaoweza kumsababishia madhara ya kiafya.

Hospitali ya Saifee iligonga vichwa vya habari mwezi January ilipoanza shughuli zake kwa kumtibu mwanamke mmoja raia wa Misri, ambaye aliaminiwa kuwa mtu mwenye uzito mkubwa zaidi duniani akiwa na uzito wa mwili wa kilo 500.

Haki miliki ya picha SHOBHAA DE
Image caption Inspekta Daulatram Jogawat alisema uzito wa mwili wake uliongezeka kutokana na matatizo ya kiafya

Bwana Jogawat aliliambia gazeti la Hindustan Times kwamba alipata "fursa ya kwenda Mumbai kwa mara ya kwanza kwa ajili ya matibabu" kwa sababu ya ujumbe huo wa Twitter.

Aliongeza kusema kuwa uzito wa mwili ulianza kuongezeka kutokana na matatizo ya kiafya, na si kwa sababu anakula sana.

"kusema ukweli, uzito wangu haukuja kutokana na kazi yangu kwa sababu nilikuwa mwenye nguvu na mkakamavu kimwili na nilikuwa na akili ya kutatua uhalifu. Nilikuwa nalipwa vyema na kazi yangu," Alisema Bwana Jogawat.

Baadaye mwandishi wa habari Shobhaa De baadae alitetea ujumbe wake wa Twitter, akisema kuwa azma yake haikuwa kumuudhi yeyote.