Donald Trump na Uhuru Kenyatta wazungumza kwa Simu

Donald Trump
Image caption Rais wa Marekani, Donald Trump na mwenzake wa Kenya, Uhuru Kenyatta wazungumza kuhusu uhusiano wa mataifa hayo mawili

Ikulu ya Nairobi imethibitisha kuwa Rais wa Marekani Donald Trump amezungumza kwa njia ya simu na Rais Uhuru Kenyatta juu ya kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.

Taarifa inasema viongozi hawa wawili walijadili juu ya ushirikiano wa kiuchumi na ushirikiano wa pamoja katika kupambana na ugaidi na masuala mengine ya usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Rais Trump ameutambua mchango wa Kenya katika kuchangia vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia na pia kujitolea kwa vikosi vya Kenya katika mapambano dhidi ya Al Shabaab. Viongozi hawa pia wamezungumzia njia za kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji katika Kenya na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Uhuru Kenyatta amekuwa rais wa nne wa Afrika kuzungumza na rais huyo kutoka taifa lenye uwezo mkubwa duniani.

Kati ya marais wa Afrika aliozungumza nao kwa njia ya simu ni rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi, rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na rais wa Nigeria Muhammadu Buhari .