Rais Muhammadu Buhari awasili Nigeria

Rais wa Nigeria awasili nchini humo baada ya likizo ya wiki kadhaa nchini Uingereza
Image caption Rais wa Nigeria awasili nchini humo baada ya likizo ya wiki kadhaa nchini Uingereza

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amerudi nyumbani baada ya kuwa katika ziara ya matibabu nchini Uingereza na uvumi kuhusu afya yake kwa wiki kadhaa.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 74 ambaye aliwasili kupitia uwanja wa ndege wa kijeshi wa Kaduna nchini humo sasa yuko katika mji mkuu Abuja kulingana na msaidizi wake ambaye alichapisha ujumbe katika mtandao wake wa Twitter.

Kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi aliondoka nchini Nigeria tarehe 19 Januari na amekuwa akifanyiwa ukaguzi wa kimatibabu mjini London.

Maelezo ya afya yake hayajatolewa ,lakini kulingana na ujumbe huo wa Twitter kutoka kwa msaidizi wake Bashir Ahmed, rais amesema kuwa: Nafurahia nimerudi,nahisi vyema zaidi sasa.

Bwana Buhari alishukia katika uwanja wa ndege wa kaduna kwa kuwa uwanja wa ndege wa mji mkuu wa Abuja umefungwa kwa muda ukifanyiwa ukarabati.

Taarifa rasmi siku ya Alhamisi ilisema kuwa rais Buhari aliondoka nchini Nigeria kwa likizo ambapo pia alifanyiwa ukaguzi wa matibabu.

Likizo hiyo iliongezwa muda kutokana na ushari wa daktari wa kumfanyia vipimo zaid na kumpumzisha.

Wakosoaji wa rais sasa wanahoji iwapo afya yake inamruhusu kuongoza taifa hilo ,kulingana na mwandishi wa BBC Martin Patience kutoka Lagos.

Chama rasmi cha upinzani cha Peoples Democratic Party PDP kimetaka kuwepo kwa uwazi kuhusu afya ya rais.

Taifa hilo kwa sasa linakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi kufuatia kuanguka kwa bei ya mafuta ambayo ndio tegemeo lake la kiuchumi.

Ni mara ya pili chini ya kipindi cha mwaka mmoja kwamba rais Buhari aliyeshinda uchaguzi 2015 amepatiwa matibabu ngambo.

Mnamo mwezi Juni alihudumia kipindi cha wiki mbili nchini Uingereza kwa matibabu kwa mambukizi ya sikio.

Ni maelezo machache yaliotolewa kwa umma kuhusu likizo yake nchini Uingereza lakini alipigwa picha siku ya Alhamisi akikutana na kiongozi wakuu wa dini wa kanisa Anglikana Askofu mkuu wa Cantebury Justin Welby.