India yaongeza mara dufu likizo ya wanawake kujifungua hadi wiki 26

India yaongeza mara dufu likizo ya wanawake kujifungua Haki miliki ya picha AFP
Image caption India yaongeza mara dufu likizo ya wanawake kujifungua

Bunge la India limepitisha sheria ambayo inaongeza likizo ya akina mama kujifungua kutoka wiki 12 hadi wiki 26.

Sheria hiyo mpya itatumika kwenye mashirika yote yenye wafanyakazi zaidi ya 10.

Waziri wa Leba Bandaru Dattatreya, amesema kuwa sheria hiyo ni zawadi kwa wanawake.

Sasa India ndiyo ya tatu kwa kuwapa wanawake muda mrefu zaidi wa kujifungua baada ya Canada na Norway ambazo huwapa wanawake wiki 50 na 44 mtawalia.

Mswada huo uliidhinishwa kwanza na bunge la juu la India mwaka uliopita, lakini ukawa sheria baada ya bunge la chini kuupitisha siku ya Alhamisi

Hata hivyo wanawake watapewa tu likizo hiyo ya wiki 26 wakati wa kujifungua watoto wawili wa kwanza, baada ya hapo watakuwa wakipewa wiki 12.

Wanaharakati wanasema kuwa sheria hiyo itachangia wanawake zaidi kuendeleza taaluma zao baada ya kujifungua.

Hata hivyo baadhi ya wakasoaji wanasema kuwa sheria hiyo itaathiri maamuzi ya makampuni wakati wa ajira.