Chama cha Modi BJP kushinda jimbo muhimu

Waziri mkuu wa India Narendra Modi Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Waziri mkuu wa India Narendra Modi

Matokeo ya mapema katika uchaguzi wa kimaeneo nchini India yanaashiria kwamba chama cha waziri mkuu wa India Narendra Modi huenda kikaibuka na ushindi mkubwa.

Chama hicho, BJP, huenda kikaibuka na ushindi mkubwa katika jimbo muhimu la kisiasa lililo na watu wengii zaidi nchini humo, Uttar Pradesh.

Uchaguzi huo unaonekana kama kura ya maoni kwa waziri mkuu Narendra Modi, kutokana na hatua yake tatanishi ya kuondoa noti zilizo na thamani kubwa nchini humo mwezi Novemba.

Ushindi katika jimbo hilo utaimarisha nafasi yake ya kutwaa ushindi mwingine katika uchaguzi wa ubunge mwaka 2019.

Maoni yanaonyesha kuwa BJP pia kinatarajiwa kushinda jimbo la kaskazini la Uttarakhand.

Chama cha upinzani kinaongoza katika majimbo ya Punjab na Manipur.

Bwana Modi amekuwa akiongoza mipango ya uchaguzi na kampeni kali akiahidi kuimarisha uchumi na kukabiliana na ufisadi.

Bwana Modi pia aliunga mkono hatua yake ya kuondoa noti zenye thamani kubwa ikiwa ni asilimia 86 fedha zake kama nji ya kukabiliana na ufisadi.

Kiongozi wa chama cha Samajwadi, Akhilesh Yadav alipinga hatua hiyo na kuwaambia wapiga kura kwamba Modi alichukua fedha kutoka kwa mifuko ya raia na kuumiza biashara katika jimbo hilo.