Rais Buhari aanza kazi rasmi

Rais Buhari aanza kazi rasmi Haki miliki ya picha BUHARI/TWITTER
Image caption Rais Buhari aanza kazi rasmi

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, amerudi kazini leo baada ya kurejea nyumbani wiki iliyopita kutoka mjini London, ambapo amekuwa kwenye likizo ya matibabu.

Kwenye akaunti yake ya mtandao wa Twitter, Buhari aliandika kuwa amerudi rasmi kazini kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi aliondoka nchini Nigeria tarehe 19 Januari, na amekuwa kwenye likizo kimatibabu mjini London.

Likizo hiyo iliongezwa muda kutokana na ushauri wa daktari wa kumfanyia uchungzi zaidi na kumpumzisha.

Wakosoaji wa rais wamekuwa wakihoji iwapo afya yake inamruhusu kuongoza taifa hilo ,kulingana na mwandishi wa BBC Martin Patience kutoka Lagos.

Chama rasmi cha upinzani cha Peoples Democratic Party PDP kimetaka kuwepo kwa uwazi kuhusu afya ya rais.

Taifa hilo kwa sasa linakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi kufuatia kuanguka kwa bei ya mafuta ambayo ndio tegemeo lake la kiuchumi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Buhari alirejea Nigeria wiki iliyopita