Kiongozi wa Upinzani Niger ahukumiwa kifungo gerezani

Wanasheria wa Hama Amadou wanasema kesi yake ni ya kisiasa Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanasheria wa Hama Amadou wanasema kesi yake ni ya kisiasa

Mahakama nchini Niger imemuhukumu kifungo gerezani kiongozi wa upinzani nchini humo anayeishi uhamishoni.

Hama Amadou amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kwa kosa la kufanya biashara ya magendo ya kusafirisha watoto.

Amekutwa na hatia ya kununua watoto wachanga kutoka nchi jirani ya Nigeria.

Wakati hukumu hiyo ikitolewa, Amadou hakuwepo mahakamani na kila mara alikuwa akikanusha tuhuma hizo na kuzielezea kuwa ni za kisiasa.

Mawakili wake pia hawakuwepo mahakamani wakati hukumu hiyo ikitolewa.

Hama Amadou aliibuka mshindi wa pili katika uchaguzi wa Rais uliofanyika mwaka jana nchini humo.

Alikamatwa na kutokana na sababu za afya aliachiwa huru mwaka jana, hali iliyomfanya kukimbilia Ufaransa.