Trump hajui apeleke wapi mshahara wake wa dola 400,000

Donald Trump Haki miliki ya picha AP

Msemaji wa ikulu ya White House amesema Rais Donald Trump atatoa mshahara wake kama hisani kwa mashirika yanayosaidia wasiojiweza katika jamii.

Sean Spicer amesema anataka waadhishi wa habari wanaoripoti taarifa kuhusu White House na Rais wa Marekani wamsaidie kuchagua nani wanafaa kupewa pesa hizo.

Mshahara wa Bw Trump utakuwa umefikia dola 400,000 kufikia mwisho wa mwaka.

Wakati wa kampeni za urais, Bw Trump alisema kwamba hakupanga kupokea mshahara wake na kwamba badala yake angepokea dola moja pekee ambayo ni lazima kisheria.

Alikosolewa wakati wa kampeni baada ya taarifa kuibuka kwamba alikuwa ametoa kiwango kidogo sana cha pesa kama hisani licha ya utajiri wake mkubwa.

Kuna viongozi wengine walioukataa mshahara?

Bw Trump si kiongozi wa kwanza wa Marekani kukataa mshahara.

Herbert Hoover, aliyekuwa ametajirika kupitia biashara ya madini kabla ya kuingia madarakani, na John F Kennedy, aliyerithi utajiri mwingi, wote walikataa kupokea mashahara na badala yake wakatoa pesa hizo zisaidie wasiojiweza katika jamii.

Haki miliki ya picha PA
Image caption JFK alitoka familia ya viongozi mashuhuri karne ya 20 nchini Marekani

Meya wa zamani Michael Bloomberg, gavana wa zamani wa California Arnold Schwarzenegger na gavana wa zamani wa Massachusetts Mitt Romney pia walikataa kupokea mishahara yao.

Mark Zuckerberg, mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, ndiye mfanyakazi anayelipwa mshahara wa chini zaidi katika kampuni hiyo.

Aidha, ni miongoni wa CEO (Afisa Mkuu Mtendaji) wengi ambao hulipwa mshahara wa $1 pekee.

Sergey Brin na Larry Page wa Google pia wamekuwa wakilipwa $1 kwa mwongo mmoja sasa.

Larry Ellison wa Oracle pia aliukataa mshahara wake kwa miaka kadha alipokuwa CEO. Afisa mkuu mtendaji wa Hewlett Packard Enterprise (HP) Meg Whitman apia alichukua hatua sawa.

Viongozi hawa hata hivyo hujipatia pesa kupitia njia nyingine. Wengi ni kupitia hisa wanazomiliki na wengine hulipwa kwa kutegemea matokeo au mapato ya kampuni.


Viongozi wa nchi nyingine hulipwa pesa ngapi?

Licha ya $400,000, anazolipwa rais wa Marekani, pia hupewa jumla ya $50,000 ambazo huwa hazitozwi ushuru, kwa mujibu wa sheria.

Waziri mkuu wa Canada alilipwa C$340,800 (£201,202) mwaka uliopita.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alilipwa $242,000 (£193,976) naye Rais wa Ufaransa Francois Hollande akalipwa $198,700 (£158,000), kwa mujbiu wa taarifa ya CNN ya mwezi Agosti.

Bw Hollande alipunguza mashahara wake kwa 30% alipoingia madarakani mwaka 2012.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May hulipwa $186,119 (£143,462)

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May hulipwa $186,119 (£143,462) kila mwaka, ingawa thamani yake kwa dola imeshuka baada ya Uingereza kupiga kura kujiondoa EU.

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza David Cameron alishutumiwa sana alipoongeza mshahara wake kwa 10% mwaka 2015.

Hata hivyo alisema jambo la busara ni kulipwa "mshahara unaolingana na kazi".

Aliongeza kwamba kuongezewa mashahara kulimpa uwezo zaidi wa kutoa pesa za hisani na mambo mengine ya kusaidia jamii.


Wazo hili lilitoka wapi?

Mwanzilishi wa Apple Steve Jobs alivumisha wazo la mshahara wa $1 Silicon Valley baada yake kurejea katika kampuni hiyo 1997.

Wakuu wa kampuni mbalimbali wamekuwa wakikosa kupokea mishahara yao tangu Vita Vikuu vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.

Haki miliki ya picha Justin Sullivan
Image caption Mwasisi wa Apple Steve Jobs ndiye aliyepatia umaarufu wazo la mshahara wa $1

Wakuu wa kampuni, benki na viwanda mbali ambao walijitolea kutumikia nchi katika majukumu mbalimbali wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia walifahamika kama "wanaume wa dola moja kila mwaka". Kwa kuwa sheria nchini Marekani huharamisha mtu kufanya kazi bila kulipwa, viongozi hao walipokea mshahara wa $1 kutimiza matakwa ya sheria kwamba walikuwa wanalipwa.

Wazo hilo lilirejea wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ambapo wakuu wa kampuni kubwa kama vile Lockheed, Chrysler na Boeing walijitokeza kutumikia nchi kama uzalendo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii