Misaada yawasili katika miji ya Syria iliyozingirwa

Raia wa Syria bado wanahitaji misaada mbalimbali Haki miliki ya picha AP
Image caption Raia wa Syria bado wanahitaji misaada mbalimbali

Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Msalaba mwekundu zimesema msafara wa magari uliobeba misaada umewasili katika miji minne ya Syria iliyozingirwa.

Misaada hiyo inatarajiwa kugaiwa watu elfu 60 ikiwa ni mara ya kwanza toka mwezi Desemba mwaka jana.

Shirika la Msalaba mwekundu limesema usambazaji wa misaada hiyo umefika katika maeneo ya Madaya na Zabadan, yaliyo pembezoni mwa mji wa Damascus, ambayo yalizuiwa na majeshi yanayounga mkono serikali. Pamoja na miji ya Foua na Kafraya iliyoko katika jimbo la Idlib ambayo imezingirwa na waasi.

Awali mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Kevin Kennedy alisema hakuna hata msafara mmoja uliofanikiwa kugawa msaada huo mwezi uliopita.