Mifuko ya plastiki kupigwa marufuku Kenya

Hope Mwanyuma, akikusanya taka mji wa kale Mombasa Februari 5, 2013. AFP/Getty Images Haki miliki ya picha AFP

Serikali ya Kenya imetangaza kwamba itapiga marufuku uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki nchini humo.

Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa Septemba mwaka huu.

Waziri wa Mazingira na Mali Asili Prof Judi Wakhungu, kupitia ilani rasmi ya serikali, amesema serikali itapiga marufuku mifuko yote ya plastiki ambayo hutumiwa kupakia na kubebea bidhaa madukani na nyumbani.

Watetezi wa uhifadhi wa mazingira wamekuwa wakilaumu matumizi ya mifuko hiyo kwa kuchangia uharibifu wa mazingira.

Mwaka uliopita, Tanzania pia ilitangaza kwamba kuanzia Januari mwaka huu ingepiga marufuku utengenezaji, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki, ikiwemo mifuko ya plastiki ya kufungashia pombe maarufu kama viroba.

Waziri wa mazingira January Makamba aliwaambia wanahabari kwamba mifuko hiyo huchangia kuchafua mazingira na kuziba mifereji.

Baadaye, muda wa kuanza kutekelezwa kwa marufuku hiyo uliongezwa hadi mwisho wa mwezi Juni mwaka huu.

Mada zinazohusiana