Lukaku akataa kandarasi ya £140,000 kwa wiki Everton

Mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku
Image caption Mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku

Mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku amekataa kandarasi yenye faida kubwa kwake katika historia ya klabu hiyo.

Klabu hiyo ya ligi ya Uingereza ilikuwa na matumaini kwamba mchezaji huyo wa Ubelgiji ataongoza kandarasi ya miaka mitano inayoaminika kugharimu pauni 140,000 kwa wiki.

Agenti wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, Mino Raiola alisema kuwa mteja wake alikuwa na uwezekano wa asilimia 99.9 kusaini kandarasi mpya katika uwanja wa Goodison Park.

Lakini Lukaku ameambia klabu hiyo kwamba hana mpango wa kuongeza kandarasi ambayo imesalia miaka miwili kukamilika.

Lukaku hajaficha kuhusu mpango wake wa kutaka kusakata dimba la vilabu bingwa Ulaya na amehusishwa na uhamisho wa kurudi katika klabu yake ya zamani Chelsea, ambapo alijiunga na Everton kwa kitita cha pauni milioni 28 mwaka 2014.

Ombi la kandarasi ya Everton bado lipo wazi huku klabu hiyo ikisema kuwa majadiliano zaidi huenda yakapata makubaliano.

Kwa sasa hatahivyo Lukaku hajakubali kandarasi yoyote na Everton huenda ikaitisha kitita cha pauni milioni 60 kwa mchezaji huyo aliyefunga mabao 19 msimu huu.