Mwanamitindo agongwa na treni akipigwa picha Marekani

Fredzania Thompson Haki miliki ya picha Press / Psalms Funeral Home

Mwanamke wa umri wa miaka 19, ambaye alikuwa anaanza kujikuza kama mwanamitindo, aligongwa na treni na kufariki alipokuwa anapigwa picha.

Fredzania Thompson alikuwa anapigwa picha hizo zake za mitindo, ambazo zilikuwa za kwanza, kwenye reli alipogongwa na gari moshi.

Picha za Thompson, alizopigwa muda mfupi kabla ya mkasa huo kutokea Navasota, Texas, zimesambazwa na familia yake.

Polisi wanasema alikuwa mjamzito wakati huo na kwamba alikuwa anaondokea treni moja kwenye njia moja ya reli alipojipata ameingia kwenye njia ya reli ambapo kulikuwa na treni nyingine iliyokuwa inapita ambayo ilimgonga.

Gazeti la The Eagle limesema ilikuwa mara yake ya kwanza kwenda kupigwa picha za uanamitindo.

"Bila shaka, hilo jambo alililotaka kulifanya maishani," Hakamie Stevenson alisema kumhusu bintiye.

"Ndiyo shughuli aliyoanza kuifanya siku aliyokumbana na mauti yake."

Polisi wanasema bado wanafanya uchunguzi kuhusu kisa hicho.

Afisa wa polisi wa Navasota ameambia BBC kwamba hata hivyo bado hawajagundua hila yoyote.

Haki miliki ya picha Press/Psalms Funeral Home
Image caption Familia ya Fredzania imetoa picha alizopigwa kabla ya kifo chake

Ukurasa umefunguliwa katika mtandao wa GoFundMe kujaribu kuchangisha $10,000 (£8,150) za kugharimia mazishi ya Fredzania.

Kwa mujibu wa shirika la reli la Marekani (FRA), watu 813 waliuawa kwenye reli Marekani mwaka 2016.

Hilo ni ongezeko la 8.45% ukilinganisha na mwaka 2015.

Mada zinazohusiana