Msemaji wa polisi Uganda Felix Kaweesi auawa kwa kupigwa risasi

Bw Felix Kaweesi akihutubia wanahabari mjini Kasese 30 Novemba, 2016 Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Felix Kaweesi akihutubia wanahabari mjini Kasese Novemba mwaka jana

Msemaji wa jeshi la polisi nchini Uganda Felix Kaweesi amepigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana.

Taarifa zinasema Bw Kaweesi ameuawa baada ya gari lake kumiminiwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa anaondoka kwake nyumbani Kulambiro, Kisaasi kaskazini mashariki mwa mji mkuu Kampala.

Walinzi wake wawili walioandamana naye pia wameuawa.

Bw Kaweesi aliteuliwa kuwa msemaji wa polisi Agosti mwaka jana.

Taarifa zinasema alikuwa njiani kwenda kuwahutubia wanafunzi katika chuo kikuu cha Uganda Christian University alipokumbana na mauti yake. Wanafunzi walikuwa tayari wamekusanyika ukumbini katika chuo hicho.

Miili ya watatu hao imepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mulago.

Mada zinazohusiana