Trump na Merkel watofautiana kuhusu uhamiaji

Trump na Angela Merkel wa Ujerumani
Image caption Trump na Angela Merkel wa Ujerumani

Rais wa Marekani Donald Trump amekutana na chansela wa Ujerumani Angela Merkel katika kikao cha kwanza cha ana kwa ana kwa majadiliano lakini imebainika wazi katika mkutano na waandishi habari kwamba wametofautiana kuhusu maswala ya uhamiaji, uhusiano wao na Urusi na hata biashara ya kimataifa ambapo Donald Trump alidai Marekani imekuwa ikipunjwa katika mikataba ya kibiashara iliyoweka saini.

Amesema sera ambayo amekuwa akiinadi si ya kujitenga bali ni kuelezea kwamba Marekani imekuwa ikionewa na hivyo kutafuta usawa wa haki katika biashara

Kwa upande wake Bi Merkel amehimiza faida za kuendeleza biashara huru ya kimataifa.

Pia ametoa wito wakimbizi watendewe haki kwa kuwa na uwazi katika kushughulikia maswala yao.

Japo viongozi hao wawili walijitahidi, ni dhahiri bado kuna ukakasi katika uhusiano wao kutokana na jinsi Trump alivyomsema bi Merkel vibaya katika hotuba zake za wakati wa kampeni.