Sekta ya Nyama matatani nchini Brazil

Brazil ni moja ya nchi zinazozalisha na kusafirisha Nyama kwa wingi duniani Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Brazil ni moja ya nchi zinazozalisha na kusafirisha Nyama kwa wingi duniani

Rais wa Brazil, Michel Temer, amezihakikishia nchi za kigeni kuwa , kashfa iliyokumba sekta ya Nyama chini mwake, haina maana kuwa bidhaa zake si salama.

Rais Temer amewaambia mabalozi kuwa nchi yake bado imeendelea kuzalisha nyama yenye ubora, ingawa kumekuwa na shutuma kuwa viwanda vyake vikubwa vitatu vimekuwa vikiuza nyama iliyooza kwa miaka mingi.

Serikali ya Brazil ina wasiwasi kuwa Marekani, China na nchi za Umoja wa Ulaya zinaweza kupiga marufuku kuingiza nyama kutoka Brazil baada ya shutuma hizo za kushtua zilizojitokeza siku ya Ijumaa.

Polisi nchini humo walifanya ukaguzi nchi nzima na kushutumu makampuni ya ufungaji nyama JBS, BRF na makapuni mengine madogo madogo kwa kuuza nyama isiyo salama, kuku na bidhaa nyingine za nyama.

Zaidi ya wafanyakazi 30 wa serikali waliokuwa na jukumu la kukagua vitendo hivyo wanachunguzwa kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.