Ukiwa na iPhone usitamke 108

Siri katika iphone Haki miliki ya picha Getty Images

Watu wenye kufanyia wengine mzaha wamekuwa wakiwahadaa wanaotumia simu za iPhone kutamka 108 kwenye huduma ya kutambua sauti ya Siri.

Bila kujua, wamekuwa wakihadaiwa kupiga simu kwa polisi na huduma za dharura.

108 ni sawa na 999 nchini India, hivyo Siri inafasiri hatua hiyo kama jaribio la anayetumia simu kupiga simu ya dharura.

Na hivyo, hilo linaifanya kupiga mara moja simu ya dharura hadi kwa polisi au maafisa wa huduma za dharura.

Kufanyia mzaha watu sana huwa hakuna madhara, lakini katika hili wanawafanya watu kupotezea muda maafisa wa kushughulikia dharura.

Usipojihadhari, katika nchi nyingi kuna sheria inayotoa adhabu kwa watu wanaopotezea muda maafisa wa dharura kwa kupiga simu bila kuwa na tukio lolote la kupiga ripoti.

Kuna wengine wanaozidi katika utani huu, kwa kuwashauri wenye simu "kufunga macho sekunde tano" wanaposoma 108.

Siri kawaida hukupa sekunde tano kubadilisha mawazo kabla ya kutekeleza agizo ulilolitoa.

Hii ina maana kwamba wenye kupiga 108 hawatafahamu kwamba wanapiga simu kwa huduma za dharura na simu zao zitaunganishwa kabla yao kugundua.

Nchini England na Wales, unaweza ukatozwa faini ya hadi £80.

Badala ya kufanya mzaha kama huo, unaweza kujifurahisha kwa kuitaka Siri ikufanyie jambo litakalokusisimua. Mfano, "Sifuri ukigawa na sifuri, jibu lake ni?"

Siri hukujibu: "Fikiria una biskuti sifuri na unagawia kwa kiwango sawa marafiki sifuri. Kila mtu atapata biskuti ngapi? Waona? Haileti maana hata kidogo. Na Cookie Monster anasikitisha kwamba hakuna biskuti, na unahuzunika kwamba hauna marafiki."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii