Trump na Urusi: Wakuu wa ujasusi Marekani kutoa ushahidi

James ComeyJanuari 2017 Haki miliki ya picha AP
Image caption Mkurugenzi wa FBI James Comey atazungumzia tuhuma za uhusiano kati ya Urusi na maafisa wa kampeni wa Trump

Wakuu wa mashirika mawili makuu ya ujasusi Marekani wanatarajiwa kutoa ushahidi kwa kamati za Bunge la Congress kuhusu madai kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani mwaka jana.

Pia, watatoa ushahidi kuhusu tuhuma kwamba kulikuwa na ushirikiano na mawasiliano kati ya Urusi na maafisa wa kampeni wa Rais Donald Trump.

Kadhalika, wataangazia tuhuma zilizotolewa na Bw Trump kwamba simu zake zilidukuliwa na mtangulizi wake Barack Obama.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Uchunguzi wa Jinai la FBI James Comey na mkuu wa Idara ya Taifa ya Usalama Mike Rogers watatoa ushahidi katika kikao nadra sana cha wazi cha kamati ya bunge kuhusu ujasusi.

Bw Trump ametaja uchunguzi huo kuwa usio wa haki.

Urusi imekanusha tuhuma kwamba lijaribu kuingilia uchaguzi wa urais Marekani.

Madai yaliyotolewa

Januari, mashirika ya ujasusi ya Marekani ,yalisema kuwa wadukuzi waliosaidiwa na Urusi, walidukua akaunti za barua pepe za maafisa wa vyeo vya juu wa chama cha Democrat na kufichua taarifa za aibu, ili kumsaidia bwana Trump kumshinda Hillary Clinton.

Ripoti ya mashirika ya CIA,FBI na NSA ilisema kuwa kiongozi wa Urusi Vladimir Putin, aliamrisha kufanywa kampeni ya kushawishi uchaguzi huo.

Tangu wakati huo Trump amekumbwa na lawama kuwa timu yake ya kampeni ilikuwa na ushirikiano na maafisa wa Urusi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Davin Nunes(kulia) mwenyekiti wa kamati ya ujususi pamoja na afisa wa Democrat Adam Schiff,

Afisa wa Republican Davin Nunes, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ujasusi pamoja na afisa wa Democrat Adam Schiff, wanaongoza uchunguzi wa madai hayo.

Bwana Nunes siku ya Jumapili, alisema kuwa hajaona ushahidi wowote unaoonyesha kuwa Urusi iliingilia kampeni ya Trump.

Naye mkurugenzi wa zamani wa idara ya kitaifa ya ujasusi James Clapper, naye amesema kuwa hakuna ushahidi wowote kuonyesha kuwa Urusi ilihusika.