Korea Kusini yalalamika kuhusu China kwa WTO

Mitambo ya Marekani ya THAAD inayowekwa nchini Korea Kusini imeighadhabisha China Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mitambo ya Marekani ya THAAD inayowekwa nchini Korea Kusini imeighadhabisha China

Korea Kusini imetoa wito kwa Shirika la Biashara Duniani WTO, kubaini ikiwa serikali ya China inayatendea vyema makampuni ya Korea Kusini.

Korea Kusini inadai kuwa China inalipiza kwa njia ya kiuchumi, hatua ya Korea Kusini ya kuruhusu kuweka kwa mitambo ya makombora ya kujikinga ya Marekani.

Waziri wa biashara nchini Korea Kusini Joo Hyung-hwan, aliliambia bunge kuwa huenda China inakiuka baadhi ya makubaliano ya kibiashara.

China inapinga kuwekwa kwa mitambo hiyo ya kujikinga, ikidai kuwa itaathiri usalama wa eneo hilo na kuiruhusu Marekani kuifanyia ujasusi.

Marekani na Korea Kusini zinasema kuwa mitambo hiyo inayofahamika kama (Thaad), imeundwa kuzuia vitisho kutoka Korea Kaskazini.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maduka ya Lotte Mart ni baadhi ya yale yaliyolengwa

Mitambo hiyo imezua kuwepo msukosuko kati ya Korea Kusini na China, ambayo ni mshirika mkubwa wa kibiashara na Korea Kusini.

Korea Kusini ilitoa malalamiko hayo kwa WTO siku ya Ijumaa.

Viongozi wa China wamelalamikia kuweka mitambo hiyo.

Mzozo huo umesababisha hatua kadha za kiuchumi dhidi ya Korea Kusini.

Mamlaka ya utalii nchini China imewaamrisha maajenti wa usafiri kuacha kutoa huduma kwa Korea Kusini kuanzia tarehe 15 mwezi Machi, kwa mujibu wa shirika la utalii la Korea Kusini.