Madaktari wa Tanzania wakataa kwenda Kenya

Cleopha Mailu
Image caption Waziri wa afya Cleopha Mailu alipotembelea hospitali ya taifa ya Kenyatta, Nairobi

Chama cha Madaktari nchini Tanzania kimepinga mpango wa kuwatuma madaktari 500 nchini Kenya wakisema Tanzania ina upungufu mkubwa wa madaktari.

Hii inafuatia makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Kenya mwishoni mwa wiki ambapo madaktari wapatao 500 watapata ajira nchini Kenya.

Kenya imeshuhudia mgomo wa madaktari uliomalizika wiki jana baada ya mgomo huo kudumu kwa siku 100.

Miongoni mwa mengine, maafisa wa MAT wamesema wanahitaji ufafanuzi kuhusu ni kwa nini Serikali ya Kenya imeshindwa kuajiri Madaktari wake na kuanza kutafuta Madaktari kutoka Tanzania huku ikizingatiwa kwamba malipo ya Madaktari wa Tanzania yatakuwa makubwa zaidi ya wenyeji.

Aidha, mbona ombi hili limefanyika kipindi cha mgomo, na utekelezaji wake umekuja siku chache baada ya kuweka makubaliano ya kusitisha mgomo.

"Kwa nini suala hili linafanyika wakati wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu 2017? Ni nani atawajibika katika suala la usalama wa raia wetu, ikizingatiwa kwamba tayari kuna viashiria vya chuki, na ikizingatia Kenya bado ina changamoto za kiusalama," taarifa kutoka kwa chama hicho ilisema.

Chama hicho pia kinataka kujua ni kwa jinsi gani Madaktari wataweza kufanya kazi bila kukamilisha taratibu za kisheria kama vile kufanya mitihani ya Bodi na kusajiliwa ilikupata uhalali wa kutibu.

"MAT inasisitiza kwamba ni muhimu kusitisha zoezi la kuwapeleka Madaktari wa Tanzania mpaka hapo Serikali ya Kenya itakapoanza utekelezaji wa makubaliano kati yake na Madaktari wao," chama hicho kimesema.

"Serikali ya Tanzania itafute namna ya kuwaajiri madaktari wake ili kuziba pengo kubwa la upungufu wa madaktari nchini (Tanzania)."

Serikali ya Kenya imetetea hatua yake ya kutoa nafasi za ajira kwa madakatari kutoka nji za nje kuboresha sekta ya afya. Hii ni baada ya muungano wa madaktari KMPDU, kuishtumu serikali kwa kufanya uamuzi huo na kuwapuuza matatabibu wake wasio na ajira.

Waziri wa afya Cleopha Mailu aliyezungumza baada ya kuzuru hospitali kuu ya taifa ya Kenyatta mjini Nairobi Jumatatu, alipinga madai hayo na kusema kuwa matabibu wa Kenya huajiriwa wanapomaliza masomo na kuwa madakatari wasioajiriwa ni kwa hiari yao.

"Si ukweli kuwa tumewapuuza madaktari wetu wasio na ajira. Madaktari wa Kenya wakitoka shule, wanaajiriwa, yule ambaye yuko barabarani na hana ajira, ni jukumu lake, au ni hiari yake yeye mwenyewe. Au alitoka kwa serikali akaenda hospitali za kibinafsi".

Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania
Image caption Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Waziri wa Afya kutoka Kenya Dkt Cleopa Mailu mara baada ya kumaliza mazungumzo yao

Aidha, Waziri huyo, amewahakikishia madaktari kutoka nchini jirani kama vile Tanzania, kuwa hawatahitajika kupitia taratibu kama vile kutahiniwa. Hii ni baada ya uvumi kuenea kuwa madaktari hao wangelazimika kufanya mtihani kama inavyohitajika.

"Daktari wa Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi wanaweza kufanya kazi mahali popote bila kufanya mtihani na bila kudhulumiwa; kwa sababu shule zote zinakaguliwa pamoja, na wana mtala sawa," alisema.

Kenya imeahidi kuwa itaendelea kuwasaka madaktari zaidi kutoka mataifa ya afrika na mataifa mengine ili kufanuikisha huduma bora. Sekta ya afya nchini humo iliathirika zaidi baada ya madaktari kugoma kwa siku mia moja na kulemaza utoaji wa huduma za afya nchini humo.

Hata hivyo, shughuli za kawaida zimerejea katika hospiali hizo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii