Teknolojia kuwasaidia wakulima wa miwa

Image caption Baadhi ya wakulima wa zao muwa wilayani Kilombero mkoani Morogoro

Idadi kubwa ya wakazi wa wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro wanajulikana kwa ukulima hasa wa zao la mpunga na muwa kwa ajili ya kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wakulima hawa walianza kukata tamaa ya ukulima huku wengine wakijaribu kufanya shughuli mbadala kama vile kujiingiza katika biashara ndogo ndogo. Hii ni baada ya mbegu za miwa walizokuwa wakitumia kupoteza ubora wake, na matokeo yake kushindwa kustahamili mabadiliko ya tabia nchi na hatimae kuvamiwa na magonjwa. Masoud Mohamed Mshame ambae ni mkulima wa miwa kutoka wilayani humo anakiri kwamba kila mwaka, mavuno yalikuwa yakipungua.

"Kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa, mwaka jana na mwaka juzi, tulivuna mapato ya chini tofauti na kipato tulichokuwa tunategemea siku za nyuma. Kwa miaka mitatu iliyopita, tulikuwa tunavuna kuanzia tani 30. Ilipofika mwaka jana, tulivuna hadi tani 20 na chini ya hapo," amesema Masoud.

Hivi sasa hali imeanza kubadilika. Baadhi ya wakulima wanaonekana kujawa na hamasa na matumaini ya kufanya vizuri katika kilimo. Hii ni baada ya kufikiwa na mradi wa endelevu maarufu kama SUSTAIN ambao umejikita zaidi katika kuzalisha mbegu za miwa ambazo baada ya kufanyiwa utafiti na Kituo cha Utafiti wa Miwa Kibaha, imethibitika kwamba zina ubora na uwezo wa kustahamili ukame.

Morogoro
Image caption Mkulima wa zao la muwa akiwa shambani

Mradi huu una wadau mbalimbali, miongoni mwao ni Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori Afrika ( The African Wildlife Foundation - AWF), ukishirikiana na Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, pamoja na Kituo cha Utafiti wa Miwa Kibaha.

Mpaka sasa takriban wakulima elfu moja, huku asilimia arobaini kati yao wakiwa ni wanawake, tayari wapo katika mpango wa mashamba darasa ya kilimo bora cha miwa ambayo yamewapa muongozo katika kuboresha kilimo hicho na kutunza miwa shambani, hali inayotarajiwa kuongeza mavuno na kufikia hadi tani 70 za miwa kwa hekta tofauti. Hii ni tofauti na awali ambapo baadhi ya wakulima wanakiri kupata kiwango kidogo.

Kilombero
Image caption Asilimia 40 ya wanawake wamenufaika na mradi wa mafunzo ya shamba darasa ya ukulima wa muwa wilayani Kilombero

Mbegu bora hupatikana kwenye mashamba makubwa ya kiwanda cha Kilombero, ambapo kabla ya kupandwa, hupitia teknolojia maalum ya kuchemshwa katika maji yenye dawa hadi kufikia nyuzi joto hamsini kwa lengo la kuzuia kushambuliwa na magonjwa kama vile Smart.

"Tunachokifanya hapa ni kuhakikisha kwamba tunaitibu hii mbegu kabla ya kuipanda ili kuhakikisha kwamba iko salama kutokana na wadudu na magonjwa," amefafanua mmoja wa wataalam wa mbegu katika kiwanda cha Sukari cha Kilombero.

Kwa mujibu wa watafiti, iwapo vitalu vya mbegu vitahudumiwa kitaalamu shambani, basi kuna uwezekano mkubwa wa kudumu hadi miaka nane mpaka kumi.

Hata hivyo, kilimo cha miwa ni biashara ambayo inahitaji maji mengi na mbolea ya kutosha. Pastor Magingi ambae ni meneja mradi-Sustain-Africa anasema wameamua kujikita zaidi katika kuwasaidia wakulima wadogo wadogo, ili wawe na kipato cha uhakika, hivyo kupunguza uwezekano wa kuharibu misitu inayowazunguka.

Image caption Kituo cha maandalizi ya mbegu za muwa katika kiwanda cha sukari cha Kilombero, mkoani Morogoro

Tanzania ina viwanda vikuu vinne vya sukari, na kumekuwa na mpango wa kuongeza uzalishaji sukari kufikia tani laki tatu kabla ya mwaka 2020. Lakini, wakati huo huo, wachambuzi wa mambo, wanahisi kabla ya lengo hilo kuweza kufikiwa, baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la muwa, zinahitaji kufanyiwa kazi ili kuongeza uzalishaji.