Bilionea Mmarekani David Rockefeller afariki

David Rockefeller Haki miliki ya picha AP
Image caption David Rockefeller alikuwa mwanawe John D Rockefeller Jr

Bilionea Mmarekani anayefahamika pia kwa kutoa pesa za hisani kuwasaidia wasiojiweza David Rockefeller amefariki dunia akiwa usingizini nyumbani kwake Poncantico Hills, New York.

Alikuwa na umri wa miaka 101.

Bw Rockefeller alikuwa wa mwisho wa kizazi chake cha familia hiyo maarufu nchini Marekani.

Alikuwa mjukuu wa mwanzilishi wa kampuni ya Standard Oil John D Rockefeller.

Mzee huyo ndiye aliyekuwa anasimamia mali na biashara za familia hiyo, pamoja na miradi yake ya kusaidia jamii.

Alikuwa kijana wa kiume mdogo zaidi kati ya wana watano wa kiume wa John D Rockefeller Jr.

Ingawa hakuwahi kutafuta wadhifa wowote wa kisiasa, kaka zake wawili walihudumu serikali.

Nelson Rockefeller alihudumu kama gavana wa New York na kwa muda kama Makamu wa Rais wa Marekani.

Winthrop Rockefeller naye alikuwa gavana wa Arkansas.

Haki miliki ya picha George HW Bush
Image caption Rais wa zamani wa Marekani George HW Bush amesema amehuzunishwa sana kwa kumpoteza rafiki yake mzuri sana

David Rockefeller alihitimu kutoka chuo kikuu cha Harvard mwaka 1936 na akapokea shahada ya uzamifu katika uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Chicago mwaka 1940.

Alitumikia jeshi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na baadaye akafanya kazi katika benki ya Chase Bank, ambayo baadaye ilikuwa benki ya JP Morgan Chase.

Bw Rockefeller alimiliki kazi za sanaa za thamani ya $500m (£404m).

Alipokuwa anasherehekea kutimiza miaka 100 mwaka 2015, alitoa ardhi ya ekari 1,000 kwa mbuga ya taifa katika jimbo la Maine.

Juhudi zake za kusaidia jamii zilimfanya kutunukiwa Nishani ya Uhuru ya Rais mwaka 1998.

Alikuwa na watoto wanne - David Jr, Richard, Abby, Neva, Margaret na Eileen.

Mkewe Margaret (jina lake la kuzaliwa McGrath) alifariki 1996.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii