Msaidizi wa zamani wa Trump, Paul Manafort, adaiwa kuficha malipo ya $750,000

Paul Manafort. Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Paul Manafort amekiri kwamba alikuwa mshauri wa rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovych

Mwenyekiti wa zamani wa kampeni wa Rais Donald Trump Paul Manafort anakabiliwa na tuhuma mpya, kwamba alilipwa pesa kisiri kutoka Ukraine.

Mbunge wa Serhiy Leshchenko amesema ana ushahidi kwamba Bw Manafort alijaribu kuficha $750,000 (£600,800) alizolipwa na chama kinachounga mkono Urusi mwaka 2009.

Msemaji wa Bw Manafort amekanusha tuhuma hizo na kusema "hazina msingi".

Bw Manafort alikuwa mshauri wa rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovych.

Amekanusha kupokea malipo yoyote ya kifedha.

Alilazimishwa kujiuzulu kama mwenyekiti wa kampeni wa Bw Trump mwezi Agosti mwaka jana baada ya kufichuliwa kwa uhusiano kati yake na Bw Yanukovych.

Bw Manafort ni mmoja wa washirika kadha wa Rais Trump ambao wanachunguzwa kuhusu uwezekano kwamba waliwasiliana na maafisa wa Urusi wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais nchini Marekani mwaka jana.

Jumatatu, mkurugenzi wa idara ya uchunguzi wa jinai Marekani (FBI) James Comey alithibitisha kwa mara ya kwanza kwamba idara hiyo inachunguza tuhuma kwamba Urusi iliingilia uchaguzi huo wa Marekani.

Jumanne, Bw Leshchenko, ambaye ni mwandishi mpelelezi wa zamani, alichapisha risiti ambayo inadaiwa kutiwa saini na Bw Manafort inayoonesha kwamba alipokea malipo ya $750,000 kama malipo kwa kampuni kwa jina Davis Manafort kwa uuzaji wa kompyuta.

Fedha hizo zilitoka kwa kampuni iliyosajiliwa Belize, kupitia benki nyingine iliyopo Kyrgyzstan.

Bw Yanukovych aliondolewa madarakani kupitia maandamano makubwa Ukraine mwaka 2014.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii