Tanzania: Waziri Nnauye aomba subira kuhusu ripoti ya uvamizi Clouds

Kamera za CCTV zinamuonyesha mwanamume mwenye kofia akiingia studioni akiwa anasindikizwa na polisi waliojihami Haki miliki ya picha CMG
Image caption Kamera za CCTV zinamuonyesha mwanamume mwenye kofia akiingia studioni akiwa anasindikizwa na polisi waliojihami

Waziri wa habari nchini Tanzania Nape Nnauye amewaomba wananchi nchini humo kuwa na subira kuhusu kutolewa kwa ripoti ya uchunguzi wa uvamizi uliotekelezwa katika studio za Clouds.

Bw Nnauye amesema kamati hiyo bado haijamaliza kazi yake na punde itakapofanya hivyo na kukamilisha ripoti husika, wananchi watafahamishwa.

"Kuna simu nyingi juu ya ripoti," ameandika kwenye Twitter.

"Nawaomba tutulie Kamati wanamalizia kazi yao, ikikamilika tutataarifiwa muda na mahali nitakapokabidhiwa!"

Waziri huyo wa habari alianzisha uchunguzi baada ya mkurugenzi wa kituo hicho cha habari, Clouds Media Groups, Ruge Mutahaba kuambia wanahabari Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alivamia kituo hicho, akiwa na polisi wenye silaha.

Kamera za CCTV katika kituo hicho zinamuonesha mtu anayedaiwa kuwa kamishna wa jiji la Dar es Salaam Paul Makonda akiwa anasindikizwa na polisi waliojihami, akiingia studio.

Rais John Magufuli alisema katika hotuba yake Jumatatu alipokuwa akizindua ujenzi wa barabara ya juu eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam kuwa Bw Makonda aendelee kuchapa kazi na kwamba yeye hafanyii kazi maneno ya kwenye mitandao kwa sababu yeye ndiye rais wa nchi.

Dkt Magufuli alisema kuwa kuna baadhi ya watu wanaingilia majukumu yake wakati yeye ndiye mwenye uamuzi na kwamba hapangiwi kazi ya kufanya kwa sababu anajiamini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii