Haki ya kufa: Conway anakabiliwa na kifo kisichovumilika

Noel Conway,
Image caption Bwana Conway, kutoka Shrewsbury, alihudhuria mahakamani akiwa kwenye kiti cha walemavu, huku akiongezewa hewa ya Oksigeni.

Mwanamume mwenye ugonjwa usiopona wa unaoathiri neva za ubongo za fahamu ameiambia mahakama kuu nchini Uingereza kwamba anakabiliwa na "kifo kisichoweza kuvumiliwa " kutokana na sheria inayoharamisha watu kusaidiwa kufa.

Noel Conway, mwenye umri wa miaka 67, aliyepatikana na maradhi hayo mwezi Novemba 2014 na ambaye hatarajiwi kuishi zaidi ya miezi 12, amesema anapaswa kuwa huru kuamua kifo chake mwenyewe.

Bwana Conway, kutoka Shrewsbury, alihudhuria mahakamani akiwa kwenye kiti cha walemavu, huku akiongezewa hewa ya Oksijeni.

Kesi hiyo ni ya kwanza kusikilizwa tangu sheria ya kusaidiwa kufa ilipopingwa mwaka 2014 na 2015.

Wanakampeni wa haki ya kufa walipoteza kesi katika Mahakama Kuu mwaka 2014 na kesi hiyo ilifuatiwa na mjadala wa bunge uliomalizika kwa wabunge kukataa jaribio la kuanzishwa kwa sheria ya kusaidiwa kufa mnamo mwaka 2015.

Kikundi cha kampeni kinachojulikana kama Heshima katika Kufa kinaunga mkono azma ya kuidhinishwa kisheria ya kusaidiwa kufa.

Haki miliki ya picha NOEL CONWAY
Image caption kabla ya ugonjwa wake Noel Conway alikua mpandaji mashuhuri wa milima ya theruji

Bw Conway anataka ruhusa ya kuangaliwa upaya kwa sheria jambo ambalo litawezesha watu wazima wagonjwa mahututi au wenye maradhi yasiyopona kuweza kufanya maamuzi yao binafsi juu ya kumaliza maisha yao.

Richard Gordon, wakili ambaye wanamuwakilisha Bwana Conway, amesema: " Anasema angependa kufia katika nchi alimozaliwa na kuishi maisha yake yote.

"Amekwama katika maamuzi yake yote: Ya kutaka amalize maisha yake sasa wakati ana uwezo wa kimwili kufanya hivyo badala ya kusubiri kifo ambacho hatakuwa na udhibiti wake pale kitakapokuja."

Amesema kuwa Bwana Conway anahangaika na maamuzi haya anayolazimishiwa na vipengele vya sheria ya jinai, yanayokiuka haki zake za kibinadamu.

Anataka kurekebishwa kwa azimio la sheria ya mwaka 1961 juu ya kujiua , ya haki za Binadamu ya mwaka 1998 inayohusiana na heshima ya maisha binafsi mtu na familia pamoja na kipengele cha 14, ambacho kinamlinda mtu dhidi ya kubaguliwa.

"Ninahisi kwamba ni haki ya mtu ya kuamua ni vipi atakufa na ni lini afe''

Haki miliki ya picha FERGUS WALSH/ BBC
Image caption Noel Conway na mkewe, Carol, wakiwa nyumbani kwao Shropshire

Ikiwa majaji wataamua kwamba Bwana Conway ana kesi ya kujadiliwa , wataombwa kutaka kesi isikilizwe haraka iwezekanavyo.

Hali yake ya kiafya inamaanisha kuwa ingawa ana uwezo wa kiakili, uwezo wake wa kutembea, kuvaa nguo, kula na kujishughulikia mambo yake binafsi ni duni kwani hali yake imedhoofika vibaya.

Kwa sasa kuna vipengele vya jumla vya sheria vinavyozuia utoaji wa haki ya kusaidiwa kufa.

Bwana Conway amesema: "Ninahisi kwamba ni haki ya mtu ya kuamua ni vipi atakufa na ni lini afe. Sheria za sasa zinaninyima kufanya hivyo.

"Badala yake, Ninawekwa katika hali ya kuumia kusiko vumilika katika miezi ya mwisho ya maisha yangu. Huenda nikafa kwa kukosa hewa ama kukwama kwa chakula kooni, au ninaweza kushindwa kabisa kutembea au kuwasiliana''.

Mada zinazohusiana