Binti kama baba: Mabinti wa marais wenye mamlaka na ushawishi duniani

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ivanka Trump tayari ni mfanyabiashara na mtu binafsi maarufu

Akiwa na ofisi yake binafsi katika ikulu ya White house, Ivanka Trump ni mwanamke ambaye hadhi yake imeimarika kama mmojawapo wa wanawake wenye mamlaka makubwa katika utawala wa Donald Trump.

Ivanka mwenye umri wa miaka 35 atahudumu kama ''macho na masikio'' ya Donald Trump, lakini hatakuwa na cheo rasmi wala mshahara atakapokuwa akifanyia kazi katika jengo la West Wing ambalo ni sehemu ya White House.

Mwanamke huyo aliyefanikiwa kibiashara na ambaye ni mtu maarufu ni mwanamke wa hivi karibuni kujumuishwa katika orodha inayoongezeka ya mabinti wa hadhi ya juu ya wakuu wa nchi kote duniani.

Mwandishi wa BBC Valeria Perasso anaangazia majukumu tofauti ya baadhi ya mabinti wa marais wenye ushawishi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maryam Nawaz Sharif alikuwa na jukumu kubwa katika kampeni za kuchaguliwa tena kwa kwa baba yake

Kampeni ya familia

Maryam Nawaz Sharif, mwenye umri wa miaka 43, ni binti yake Waziri Mkuu wa Pakistani Nawaz Sharif.

Mwanzo alijihusisha na shughuli za shirika la familia la misaada, baadaye Bi Nawaz alitekeleza jukumu kubwa la kuwa meneja wa kampeni za uchaguzi katika mwaka 2003 zilizofanikisha kuchaguliwa tena kwa baba yake.

Kwa sasa anahudumu katika chama cha baba yake cha mrengo wa kulia kinachofahamika kama - Pakistan Muslim League (Nawaz).

"Amekuwa mtu wa kuangaziwa mara kwa mara," anasema mwandishi wa BBC idhaa ya Urdu Asif Farooqi, ambaye amekutana naye mara kadhaa.

"Kusema ukweli amejitokeza kama mtu mwenye mamlaka makubwa, na kama mtu atakayemrithi baba yake."

Mwaka jana jina lake lilijitokeza katika kile kilichofahamika kama - nyaraka za Panama, ambapo taarifa zilidai yeye na kaka zake wana uhusiano na sakata ya umiliki wa mali zisizofahamika katika mataifa ya kigeni na akaunti zinazotumiwa kununua mali za kifahari jijini London.

Baba yake alipuuzilia mbali shutuma hizo akitaja taarifa hizo ambazo alisema ni kazi ya watu "wanaonilenga pamoja na familia yangu kwa malengo ya kisiasa".

Shutuma hizo zinachunguzwa na Mahakama ya Juu ya Pakistan na uamuzi unatarajiwa kutangazwa wiki kadhaa zijazo .

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Binti yake tais Vradimir Putin wa Urusi Yekaterina ni mchezaji maaruru wa mashindano ya densi ya rock and roll

Densi ya Rock and Roll

Rais wa Urusi Vladimir Putin anafahamika kwa kulinda maisha yake ya kibinafsi, na ni hivi karibuni tu ambapo taarifa chache tu zilijulikana kuhusu maisha ya mabinti zake wawili.

"Maafisa wa Urusi huangalia nia yoyote ya vyombo vya habari kama jambo la kushukiwa," anasema mwandishi wa BBC wa Urusi Famil Ismailov.

"NI jukumu la waandishi wa habari wenyewe kujaribu ni wapi wanaweza kufikia kupata habari na taarifa nyingi hazijawahi kuthibitishwa na familia."

Mwaka 2015, binti mdogo wa rais Putin, Yekaterina, allijitokeza hadharani baada ya kufichuliwa kwa taarifa kuwa alikuwa akiishi mjini Moscow akitumia jina la Katerina Tikhonova.

Tangu wakati huo walifahamu kupitia ripoti za vyombo mbali mbali vya habari kwamba ameolewa na mfanya biashara Kirill Shamalov, mtoto wa kiume wa mmoja wa marafiki wa zamani wa baba yake na wawili hao wana utajiri wa thamani ya dola bilioni 2 kupitia uwekezaji katika gesi na viwanda vya petroli itokanayo na kemikali.

Sasa na umri wa miaka 30, na anaendesha miradi ya umma ya 'maendeleo ya elimu' katika Chuo Kikuu cha taifa cha Moscow.

Anaripotiwa kusimamia mikataba yenye thamani ya mamilioni ya dola na washauri wake ni washirika wa karibu wa Putin.

Tikhonova pia ni mchezaji densi mashuhuri wa densi ya sarakasi ya Rock and Roll , ambapo alichukua nafasi ya tano katika mashindano ya dunia ya mchezo huo nchini Uswizi ya mwaka 2013.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bi Dos Santos aliteuliwa na baba yake kama mkuu wa kampuni ya taifa ya Angola

"Tajiri zaidi Afrika"

Isabel dos Santos, mwenye umri wa miaka 43, ni mtoto wa kwanza wa rais mkongwe wa Angola Jose Eduardo dos Santos, ambaye ametawala nchi hiyo tangu 1979.

Anaongoza kampuni ya taifa ya mafuta -Sonangol na mwaka 2013 Jarida la Forbeslilibainisha kuwa ndiye mwanamke tajiri zaidi barani Afrika na mwanamke wa kwanza bilionea (kwa dola za Marekani) akikadiriwa kuwa na mali ya thamani ya dola Bilioni 3.2.

Bi Dos Santos ambaye alipata elimu yake nchini Uingereza pia amewekeza katika kampuni mbali mbali kama vile ya benki, mawasiliano ya simu na madini ya almasi, jambo linalomfanya kuwa mmojawapo ya wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Angola.

Ana uwekezaji zaidi katika sekta ya umeme, mafuta na gesi katika taifa la Ureno lililokuwa mkoloni wa zamani wa Angola.

Katika taifa ambalo shirika la kimataifa la kukabiliana na ufisadi Transparency International linasema ni moja ya nchi zenye ufisadi mkubwa zaidi duniani, Bi Dos Santos amekuwa akikabiliwa na ukosoaji wa mara kwa mara kwamba amepata utajiri huo kutokana na cheo cha baba yake. Ni dai ambalo washauri wake wanalipinga vikali.

"Mafanikio niliyonayo leo si jambo ambalo lilikuja mara moja", aliiambia BBC mnamo mwaka 2015.

"Ni kitu ambacho kimechukua miongo kujenga."

Haki miliki ya picha Turkish Presidency/Y. Bulbul/Anadolu Agency/Getty
Image caption Sumeyye Erdogan ameolewa na Selcuk Bayraktar, mfanyabiashara mwenye maslahi ya ulinzi

Sumeyye Erdogan, Kipenzi cha baba yake

Sumeyye Erdogan, mwenye umri wa miaka 31, ni binti mdogo zaidi wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na anaonekana kwa kiasi kikubwa kama anayependwa zaidi na baba yake.

"Baba yake humuita 'swara wangu,'" anasema Irem Koker, wa Idhaa ya BBC ya Kituryki .

"Nchini Uturuki neno hilo swara hutumiwa kuwaelezea watu wenye sura nzuri na wa thamani ."

Bi Erdogan ambaye alisomea siasa katika mataifa ya Marekani na Uingereza , alihudumu kama mshauri wa baba yake alipoongoza chama tawala cha Haki na Maendeleo (AKP) na amekuwa akimsindikiza baba yake mara kadhaa katika mikutano mbali mbali ya kidiplomasia.

Mwaka 2015 kulikuwa na fununu kwamba huenda Sumeyye atawania ubunge, lakini hakufanya hivyo.

Kwa sasa anashikilia wadhfa ambao si maarufu akiwa kama mkuu wa kikundi cha Uturuki kinachotetea haki za wanawake .

Zaidi ya kazi yake hiyo Sumeyye ameendelea kuwa mtu anayemuunga mkono wazi baba yake pamoja na serikali yake.

Haki miliki ya picha PRESIDENCY OF THE REPUBLIC OF TAJIKISTAN
Image caption Ozoda Rahmon ni mmoja kati ya watoto tisa wa rais wa Tajikistan

Mkuu wa majeshi na seneta

Akiwa na umri wa miaka 39, Zoda Rahmon, ni bintiye Emomali Rahmon, rais wa muda mrefu wa Tajikistan.

Ana Shahada ya uanasheria na alianza taaluma yake katika huduma za kibalozi, kabla ya kuwa naibu waziri wa mambo ya nje mwaka 2009.

Mnamo mwaka 2016 baba yake alimteuwa kuwa mkuu wa utawala katika ofisi ya rais na akashinda kiti cha bunge la Seneti.

Ozoda ameolewa na Jamoliddin Nuraliyev, naibu mwenyekiti wa kwanza wa Benki Kuu ya Tajikistan na wawili hao wana watoto watano.

Ndiye pekee katika familia ya Rahmon mwenye kazi ya serikali.

Mmoja kati ya watoto tisa, kaka yake mkubwa Rustam ni meya wa mji mkuu Dushanbe, na mdogo wake wa kike Rukhshona anafanya kazi katika wizara ya mambo ya nje.

Ndugu wengine wanaripotiwa kuwa na kazi za juu katika serikali na biashara, na hivyo kuifanya familia ya Rahmon kuwa miongoni mwa familia tajiri na yenye ushawishi zaidi nchini Tajikistan.

Haki miliki ya picha Johnny Nunez/ WireImage/ Getty Images
Image caption Binti yake Raul Castro Mariela ni mtetezi mkuu wa watu waliobadilisha jinsia na wapenzi wa jinsia moja

Sauti ya wenye maumbile ya kijinsia ya wachache

Kama binti wa rais wa Cuba Raul Castro, Mariela Castro ni mpwa wake hayati kiongozi mwanamapinduzi Fidel.

"Mama yake, Vilma Espin, alionekana kama mtu aliyeongoza harakati za kupigania haki za wanawake ," Liliet Heredero mwandishi wa BBC idhaa ya Mundo.

"Na sasa bintiye kwa kiasi fulani amefuata nyayo zake ."

Bi Castro ambaye alizaliwa mwaka 1962, na mtu asiyesita kutoa mawazo yake ni mbunge na anafahamika sana kwa utetezi wake wa watu wenye maumbile ya kijinsia ya wachache .

Anaongoza kituo cha kitaifa cha elimu ya ngono (Cenesex), kinachodhaminiwa na serikali mjini Havana ambacho kimekuwa na mchango mkubwa katika kubuni sera juu ya masuala kadhaa kuanzia kudhibiti HIV na Ukimwi hadi haki za wapenzi wa jinsia moja.

Alikuwa kiungo muhimu katika kampeni za kupitishwa kwa sheria mpya mwaka 2008 iliyowezesha utoaji bure wa huduma ya kubadilisha jinsia nchini Cuba

"Hata hivyo anaonelewa na wengi kama mtu mwenye utata," anasema Heredero. "Watu wengi husema ameruhusiwa kufanya anachokitaka kwa sababu tu ni binti yake rais ."

Mada zinazohusiana