Tanzania: Kamati yasema Makonda alitumia vibaya madaraka Clouds

Makonda Haki miliki ya picha Google
Image caption Rais Magufuli siku ya Jumatatu alimtaka Bw Makonda kuendelea kuchapa kazi

Kamati iliyoundwa na waziri anayeshughulikia masuala ya habari nchini Tanzania Nape Nnauye kuchunguza uvamizi wa kituo cha habari cha Clouds, imewasilisha ripoti yake leo hii kwa waziri huyo.

Miongoni mwa mambo yaliyobainika katika ripoti hiyo iliyofanyiwa kazi siku mbili ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka yanayomkabili mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda dhidi ya vyombo vya habari.

Bw Makonda anadaiwa kutotambua ukubwa wa madaraka aliyonayo na kuyatumia isivyostahili sambamba na viashiria vya uvunjifu wa amani kutokana na vitendo hivyo.

Kamati hiyo pia imetoa mapendekezo kadhaa ikiwemo mkuu huyo wa mkoa kuomba radhi kwa wafanyakazi wa chombo cha habari cha Clouds pamoja na wanahabari wote Tanzania.

Kamati hiyo inapendekeza Bw Nauye awasilishe malalamiko ya waandishi wa habari dhidi ya mkuu huyo wa mkoa kwa Rais wa Tanzania pamoja na kuanzishwa kwa uchunguzi dhidi ya polisi waliongia na silaha za moto kwenye chombo hicho cha utangazaji.

Akipokea ripoti hiyo, Bw Nnauye pamoja na kuwataka viongozi wa umma kufanya kazi kwa uweledi, ameahidi kukabidhi taarifa hiyo kwa mamlaka za juu zaidi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kutokana na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hiyo

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii