Runinga ya kidini 'yachezesha' kanda ya ngono Senegal

Runinga ya Touba nchini Senegal Haki miliki ya picha youtube
Image caption Runinga ya Touba nchini Senegal

Runinga moja ya kidini nchini Senegal imemlaumu mtu mmoja ambaye hakutajwa kwa hujuma ya kishetani iliosababisha kanda moja ya ngono kuonyeshwa hewani.

Watazamaji wa runinga ya Touba walishangazwa wakati picha hizo za ngono zilipoonekana katika runinga zao kati ya saa saba na dakika kumi na saa saba unusu siku ya Jumatatu.

Runinga hiyo ya kibinafsi awali ilikuwa imesema kuwa kulikuwa na tatizo la mitambo lililosababisha tatizo hilo.

Runinga ya Touba inaendeshwa na kundi la Waislamu kutoka Senegal la Mouride.

Chombo hicho sasa kimewasilisha malalamishi yake kwa mamlaka ili kuwasaka wahusika.

Video hiyo ya ngono ilichezeshwa wakati wa kipindi maarufu cha Tarixu Juma kwa takriban dakika 15.

''Kama chombo cha kidini, usimamizi wa Touba TV pamoja na watazamaji wake wameshangazwa na wanashtumu kitendo hiki cha kihalifu ambacho kinaonekana kuwa hujuma za kishetani dhidi ya chombo kinachojulikana kwa kupigania maadili ya kiislamu na mafunzo yake'' ,ulisema usimamizi wa Touba TV

Runinga hiyo inapeperusha vipindi vya kidini na kukuza maadili ya kiislamu na mafunzo yake.

Haijulikani ni vipi washukiwa waliweza kuingia katika mitambo ya runinga hiyo.

Touba ndio runinga ya pekee ya mji wa madhehebu ya Mouride, ambayo ina ushawishi mkubwa wa kisiasa pamoja na kiuchumi nchini Senegal.