Mama wa Uingereza akana kupanga njama dhidi ya Kagame

Violette Uwamahoro(kulia) pamoja na wakili wake
Image caption Violette Uwamahoro (Kulia ) alikamatwa tarehe 14 Februari

Mama mjamzito kutoka Uingereza amefikishwa mahakamani nchini Rwanda kujibu mashtaka ya kusambaza siri za taifa , kujaribu kumdhuru rais Paul kagame na kujaribu kuunda kundi la silaha.

Violette Uwamahoro, Mnyarwanda mwenye uraia wa Uingereza, amekana mashtaka yote dhidi yake mbele ya mahakama kuu katika mji mkuu Kigali.

Alionekana mtulivu wakati alipokuwa mahakamani, na kutabasamu alipokuwa akiondoka kutoka kwenye jengo la mahakama , ameripoti mwandishi wa habari Phocas Ndayizera kutoka mahakamani.

Alirejeshwa kwenye mahabusu ya polisi hadi pale kesi kuhusu dhamana itakaposikilizwa siku ya Jumatatu

Uwamahoro, ambaye ni muhudumu katika masuala ya vijana kutoka Leeds ambaye ana ujauzito wa miezi mitano wa mtoto wa tano, alikamatwa siku ya wapendanao -Valentine's Day baada ya kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya mazishi ya mama yake.

Mumewe Faustin Rukundo alisema kuwa mkewe amekamatwa kutokana na nafasi ya mumewe kama mwanaharakati wa kisiasa.

Mumewe ni mwanachama wa kikundi cha upinzani cha Rwandan National Congress

Mshatakiwa mwenza wa Bi Uwamahoro ambaye ni polisi alikiri mashtaka , akisema kuwa walikuwa na mawasiliano nae katika WhatsApp juu ya "njama " za kuipindua serikali.

Rais Paul Kagame amekuwa akishutumiwa na wakosoaji wake kwa kuwa na utawala wa ukandamizaji, suala ambalo analikana.

Watoto wa Bi Uwamahoro, Samuel, mwenye umri wa miaka minane, na David mwenye umri wa miaka , 10, wamemuandikia barua Waziri Mkuu wa uingereza Theresa May na Rais Paul kagame kuwaomba wamsaidie mama yao.