Waziri aliyefutwa Tanzania Nape Nnauye asema alijua kuna gharama

Huwezi kusikiliza tena
Waziri aliyefutwa Tanzania Nape Nnauye asema alijua 'angelipia gharama'

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alihuhutubia waandishi wa habari leo akiwa chini ya vyombo vya usalama na kutetea msimamo wake.

Taharuki ilitokea mara baada ya waandishi wa habari kupata taarifa kuwa kikao kilichoandaliwa na aliyekuwa waziri wa habari hakipo tena, lakini dakika chache baadae Nape aliandika katika kurasa yake ya Twitter kuwa yuko njiani na kikao kipo palepale.

Nape alipofika karibu na eneo la kikao alizuiwa na askari kutoka katika gari lake huku wakimshika kwa nguvu na kumtishia kwa kumnyooshea bunduki.

Hali hiyo ilimfanya Nape kuongea kwa hasira akitaka kujua nia ya askari hao kumnyooshea bunduki, huku kundi kubwa la waandishi wa habari wakipiga kelele wakitaka askari hao wamuachie Nape aongee.

Nape alianza kwa kusema nia yake ilikuwa ni kutaka kuwatuliza wananchi watulie kwa sababu wakati anateuliwa hakuulizwa na hata sasa ameachishwa hajaulizwa na yeye hana kinyongo na rais wake.

Ingawa aliendelea kuzungumza kwa hasira alisema haogopi chochote.

"Jana wakati narudisha ripoti kuhusu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia kituo cha habari cha habari cha Clouds, nilijua kuwa kuna gharama ya kuilipa," alisema Bw Nnauye.

"Hivyo nashangaa kwa nini vyombo vya usalama 'wanapaniki', kwa nini watu 'wanapaniki'. Nape ni mtu mdogo tu ila tuhangaike na Tanzania yetu, mimi nmesimamia ukweli tu, Kinachokutanisha watu ni ukweli na sio fitina. Vijana wenzangu wa Kitanzania simamieni ukweli".

Hata hivyo aliongeza kwa kusema kuwa lengo la kuja kuzungumza hapo ni kumshukuru rais kwa kumwamini kumpa nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Aidha, alimpongeza waziri mpya aliyechaguliwa, Dkt Harrison Mwakyembe, kwa kuwa ni mwanasheria na ana taaluma ya habari.

Image caption Waandishi wa habari wakijaribu kupata habari kutoka kwa Bw Nnauye

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii