Aliyekuwa Waziri wa habari,Tanzania Nape Nnauye apata wakati mgumu kuongea na wanahabari

Image caption Aliyekuwa waziri wa Habari,nchini Tanzania

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Nape Nnauye amezungumza na waandishi wa habari leo katika mazingira ya uangalizi wa vyombo vya usalama hali iliyozua vurugu katika maeneo ya Hotel ya Protea jijini Dar es salaam.

Taharuki ilitokea mara baada ya waandishi wa habari walipopata taarifa kuwa kikao kilichoandaliwa na aliyekuwa waziri wa habari Nape hakipo tena,lakini dakika chache baadaye Nape aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba yuko njiani na kikao kipo palepale.

Nape alipofika karibu na hotel hiyo ili azungumze na waandishi wa habari,alizuiwa na askari kutoka katika gari yake huku wakimshika kwa nguvu kama mtuhumiwa na kumtishia kwa kumnyooshea bastola.

Image caption Waandishi wa habari wakijaribu kupata habari kutoka kwa aliyekuwa waziri wa habari

Hali hiyo ilimfanya Nape kuongea kwa hasira akitaka kujua nia ya askari hao kumnyooshea bastola, huku kundi kubwa la waandishi wa habari wakipiga kelele wakitaka askari hao wamuachie Nape aongee alichopanga kuzungumza.

Nape alianza kwa kudai kuwa nia yake ilikuwa ni kutaka kuwatuliza wananchi watulie kwa sababu wakati anateuliwa hakuulizwa na hata sasa ameachishwa bila kuulizwa na kwamba huo ndiyo utaratibu na hana kinyongo na rais wake.

Ingawa aliendelea kuzungumza kwa hasira kwa kusema hakuna cha kuogopa kwa kuwa hao watu wa usalama,wanalipwa kwa kodi ya wananchi na yeye amelala porini takribani miezi 28 akipigania kurejesha heshima ya chama cha mapinduzi,CCM kurejea madarakani.

"Jana wakati narudisha ripoti kuhusu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda kuvamia kituo cha habari cha habari cha Clouds,nilijua kuwa kuna gharama ya kuilipa, hivyo nashangaa kwa nini vyombo vya usalama wanapaniki,kwa nini watu wanapaniki;Nape ni mtu mdogo tu ila tuhangaike na Tanzania yetu ,mimi nmesimamia ukweli tu.Kinachokutanisha watu ni ukweli na sio fitina,Vijana wenzangu wa kitanzania simamieni ukweli"

Hata hivyo aliongeza kwa kusema kuwa lengo la kuja kuzungumza hapo ni kumshukuru rais kwa kumwamini kumpa nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja na anampongeza sana waziri aliyechaguliwa,Dr.Harrison Mwakyembe kwa kuwa ni mwanasheria na ana taaluma ya habari.