Wahamiaji 200 wafa maji bahari ya Mediterranean

Proactiva Open Arm Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ni miili mitano ekee ambayo imepatikana

Wahamiaji zaidi ya 200 wanahofiwa kufariki baada ya boti lao kuzama kwenye bahari karibu na pwani ya Libya, shirika moja la Uhispania limesema.

Shirika hilo, Proactiva Open Arms, limesema maafisa wake walipata miili mitano ikielea karibu na boti mbili zilizokuwa zimezama, na ambazo zina uwezo wa kubeba zaidi ya watu 100 kila moja.

Afisa wa shirika hilo Laura Lanuza amesema miili ya watu hao watano waliyofanikiwa kuitoa baharini inaonesha walikuwa wanaume wa umri mdogo.

Msemaji wa kikosi cha majini cha Italia, ambacho huratibu shughuli za uokoaji, amethibitisha vifo vya watano hao.

Hata hivyo, amesema hawawezi kuthibitisha makadirio idadi ya waliofariki, kama yalivyotolewa na Proactiva kwa kuwa hawakupokea vilio vyovyote vya watu wakiomba msaada.

Bi Lanuza hata hivyo amesema wahamiaji 240 huenda walifariki kwani boti mara nyingi hujazwa watu kupita kiasi na walanguzi.

Shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM) linasema zaidi ya wahamiaji 20,000 wamefika Italia mwaka huu kufikia sasa.

Watu 559 wanaaminika kufariki au kutoweka wakiwa safari kuelekea Ulaya kupitia eneo hilo.

Miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2016, kulikuwa na wahamiaji 19,000 waliowasili Italia na vifo 350.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii