Mwanamuziki Ney wa Mitego akamatwa Tanzania

Ney wa Mitego alikamatwa kuhusiana na wimbo wake alioutoa hivi karibuni Haki miliki ya picha Ney wa Mitego/Facebook
Image caption Ney wa Mitego alikamatwa kuhusiana na wimbo wake alioutoa hivi karibuni

Jeshi la Polisi nchini Tanzania linamshikilia mwanamuziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki, alimaarufu kama Ney wa Mitego kuhusiana na wimbo wake alioutoa hivi karibuni, mwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo

Gazeti la Mwananchi linaripoti kwamba Ney wa Mitego, alikamatwa mnamo majira ya saa nane usiku wa kuamkia siku Jumapili katika mkoa wa Morogoro, kilomita 200 kutoka jijini Dar es Salaam, kwa kosa la kutoa wimbo unaoikashifu serikali

Wimbo huo mpya wa Ney wa Mitego, ulianza kusambaa katika mitandao ya kijamii wiki iliyopita huku sehemu ya maudhui ya wimbo huo ukigusia tuhuma za kughushi vyeti ambazo zimekuwa zikigonga vichwa vya habari nchini Tanzania

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Ulrich Matei alilithibitishia gazeti la Mwananchi kukamatwa kwa Ney wa Mitego na kuongeza kuwa sababu ni kosa la kutoa wimbo wenye maneno ya kashfa dhidi ya serikali.

Matei alisema Ney wa Mitego angepelekwa jijini Dar es Salaam ambako ndipo shauri lake lilipo na kuhojiwa zaidi na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa juu ya kazi zake za kisanaa