Urusi yazungumzia maandamano ya Jumapili na kuyataja kuwa uchokozi

Alexei Navalny akikamatwa mjini Moscow Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Alexei Navalny akikamatwa mjini Moscow

Urusi imezungumzia maandamano makubwa yaliyoshuhudiwa siku ya Jumapili kwa kuulaumu upinzani kwa kuvunja sheria na kusababisha ghasia .

Vijana walilipwa kushiriki maandamano hayo kwa mujibu wa msemaji wa rais , lakini ameongeza kuwa ujumbe kutoka kwa maandamano yanayoambatana na sheria utasikilizwa.

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny, ambaye ni mmoja wa mamia ya watu waliokamatwa alifikishwa mahakamani leo.

Alirejelea shutuma za ufisadi dhidi ya waziri mkuu Dmitry Medvedev.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waandamanaji walizuia basi ambamo Alexei Navalny alikuwa

Madai hayo ndiyo yalisabababisha maandamano ya siku ya Jumapili yaliyowafutia maelfu ya watu kote nchini humo ikiwemo miji ya Saint Petersburg, Vladivostok, Novosibirsk, Tomsk na miji mingine ukiwemo mji mkuu Moscow. Takriban watu 500 walikamatwa.

Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov, kwenye matamshi ya kwanza kutoka kwa urais, alisema kile walichokiona jana maeneo tofauti hasa mjini Moscow ni uchokozi na uongo.

Alisema kuwa kuwa vijana waliokuwa wameahidiwa kulipwa ikiwa wangekamatwa na polisi.

Image caption Alexei Navalny alituma picha hii kutoa mahakamani kupitia Twitter

Bwana Peskov alipongeza hatua ya vikosi vya ulinzi na kutupilia mbali wito kutoka kwa Muungano wa Ulaya wa kutaka wale waliokamatwa kuachiliwa bila kuchelewa.

Alipoulizwa na BBC ikiwa bwana Medvedev atajibu madai ya ufisadi yanayomuandama, yaliyosababisha maelfu ya watu kuingia barabarani, bwana Peskov hakujibu lolote.