Mwanamuziki Ney wa Mitego aachiliwa huru Tanzania

Wa Mitego baada ya kuachiliwa huru
Image caption Wa Mitego baada ya kuachiliwa huru

Mwanamuziki Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego, ambaye alikuwa amekamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa polisi Tanzania kuhusiana na wimbo wake, ameachiliwa huru.

Wa Mitego ameachiliwa huru saa chache baada ya Waziri wa Habari nchini Tanzania Dkt Harrison Mwakyembe kuagiza aachiliwe huru.

"Saa hizi sina kubwa la kuongea. Wimbo umeruhusiwa. Nashukuru. Nafurahi kusikia taarifa ya serikali kwamba wameruhuru wa Wapo upigwe. Upigwe kwa nguvu," amesema Wa Mitego baada ya kuachiliwa huru.

Kuhusu kuuboresha wimbo huo, amesema: "Hili nitalifanyia kazi. Siwezi kusema saa hizi ni vitu gani kwa sababu ndio nimetoka huko. Lakini nitalifanyia kazi kwa sababu tayari ni wimbo wa kila mtu, wimbo wa Watanzania, wimbo wa watu wote."

Dkt Mwakyembe hata hivyo alimtaka Ney wa Mitego auboreshe zaidi wimbo wake, kwa mujibu wa ujumbe uliopakiwa katika ukurasa Rasmi wa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania kwenye Twitter.

Sehemu ya maudhui ya wimbo huo inagusia tuhuma za kughushi vyeti ambazo zimekuwa zikigonga vichwa vya habari nchini Tanzania

Wimbo huo mpya wa Ney wa Mitego, ulianza kusambaa katika mitandao ya kijamii wiki iliyopita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Ulrich Matei alikuwa amesema mwanamuziki huyo alikamatwa kwa kosa la kutoa wimbo wenye maneno ya kashfa dhidi ya serikali.

Mapema leo, Baraza la Sanaa la Taifa Tanzania (Basata), lilikuwa limetangaza kuufungia wimbo huo kwa jina Wapo usichezwe kwenye vyombo vya habari au kutumika kwa namna yoyote ile.

"Basata linawakumbusha wasanii na wadau wote wa kazi za sanaa kuzingatia ubunifu wa hali ya juu kufanya kazi za sanaa, hata kufikisha ujumbe mbalimbali wa kufundisha, kuelimisha, kuburudisha na hata kuonya," taarifa kutoka kwa baraza hilo ilisema.

Image caption Wa Mitego baada ya kuachiliwa huru

"Baraza linawaonya wale wote wanaotumia kazi zilizopigwa marufuku, ikumbukwe kuwa kutumia kazi zilizopigwa marufuku ni ukiukwaji wa sheria za nchi (na) hatua kali zitachukuliwa juu yao."

Awali kulikuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba Rais wa Tanzania John Magufuli alikuwa ameagiza wimbo huo uendelee kuchezwa.

Haki miliki ya picha Ney wa Mitego/Facebook
Image caption Ney wa Mitego alikuwa amekamatwa kuhusiana na wimbo wake alioutoa hivi karibuni

Kiongozi wa upinzani kutoka chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe hata hivyo alionekana kukerwa na taarifa hizo.

Bw Kabwe alisema Rais hana mamlaka yoyote ya kuamua wimbo uchezwe au usichwezwe.

"Ilikuwa ni makosa kumkamata Ney na agizo la Rais halina maana pia," aliandika kwenye Twitter.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii