Nnauye: Waziri aliyefutwa asema bado anaunga mkono juhudi za Magufuli

Nnape Nauye Haki miliki ya picha NNAPE NAUYE/TWITTER

Aliyekuwa waziri wa habari, utamaduni, Sanaa na michezo nchini Tanzania Nape Nnauye amesema bado anaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kujaribu kufanikisha mageuzi nchini humo.

Bw Nnauye, akizungumza wakati wa kukabidhi rasmi afisi kwa mrithi wake Dkt Harrison Mwakyembe, kadhalika amesema ataendelea kushirikiana na wizara hiyo.

Amesema yeye ni mdau mkubwa katika sekta zilizomo chini ya wizara hiyo.

Bw Nnauye alifutwa kazi wiki iliyopita siku moja baada yake kupokea ripoti ya kamati ya uchunguzi kuhusu uvamizi uliotekelezwa na mtu anayedaiwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika studio za kituo cha habari cha kibinafsi cha Clouds.

Kamati hiyo, kwenye ripoti yake, ilionekana kumkosoa Bw Makonda na kusema alitumia vibaya mamlaka yake.

"Heshima aliyonipa mheshimiwa Rais ni kubwa mno na nitaendelea kumuunga mkono katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini," alisema Bw Nnauye, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wizara ya habari na michezo Tanzania.

Taarifa hiyo inasema Bw Nnauye ameahidi ataendelea kuwa mtiifu kwa Rais Magufuli, serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Haki miliki ya picha Habari Maelezo, Tanzania
Image caption Bw Nnauye akikabidhi rasmi afisi kwa Dkt Mwakyembe

Bw Nnauye, ambaye ni mbunge wa Mtama, alisimamia wizara hiyo kwa miezi 15.

Waziri mpya Dkt Mwakyembe amesema anategemea kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwa Bw Nnauye.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii