Simone Gbagbo aondolewa mashitaka yaliyokuwa yakimkabili

Simone aliunga mkono mumewe kung'ang'ania madaraka
Image caption Simone aliunga mkono mumewe kung'ang'ania madaraka

Mke wa aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Simone Gbagbo ameondolewa mashitaka yaliyokuwa yakimkabili juu ya vitendo vya kikatili dhidi ya binadamu.

Kesi yake ilikuwa inasikilizwa katika mji wa biashara wa Abidjan.

Mashitaka yanahusu vurugu zilizoibuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 wakati mumewe Laurent, aliyakataa matokeo ya ushindi wa Alassane Ouattara.

Kulikuwa na mapigano nchini kote wakati wapiganaji wanaomuunga mkono Gbagbo waliwashambulia wanaomuunga mkono Ouattara.

Majaji wameyatupilia mbali madai ya mwendesha mashitaka yanayodai Simone Gbagbo aliongoza vurugu hizo na alijaribu kununua silaha.

Tayari Simone anatumikia kifungo cha miaka ishirini jela kwa kuushambulia vyombo vya dola.

Mumewe anashitakiwa katika Mahakama ya kimataifa inayoshughulikia makosa ya jinai (pia uhalifu dhidi ya binadamu).