Brexit: Uingereza yaanza rasmi kujiondoa EU

Theresa May Haki miliki ya picha PA
Image caption Theresa May akitia saini barua ya kuanza kujiondoa EU

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametia saini barua ambayo itaanzisha rasmi mchakato wa kuiondoa Uingereza kutoka kwa Muungano wa Ulaya.

Barua hiyo inatoa taarifa rasmi ya kujiondoa kwa muungano huo kwa kitumia Kifungu 50 cha Mkataba wa Lisbon.

Itawasilishwa kwa rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk baadaye leo.

Kwenye taarifa kwa bunge la chini nchini Uingereza, Bi May baadaye anatarajiwa kuwaambia wabunge kwamba hatua hiyo inaashiria "wakati we taifa letu kuungana pamoja."

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na kura ya maoni iliyoandaliwa Juni mwaka jana, ambapo wapiga kura waliunga mkono kujiondoa kutoka kwa EU.

Barua ya Bi May itawasilishwa kwa Bw Tusk Jumatano mwenzo wa saa sita unusu adhuhuri saa za Uingereza na balozi wa nchi hiyo katika EU Sir Tim Barrow.

Waziri mkuu ambaye ataongoza kikao cha baraza la mawaziri asubuhi, baadaye atatoa hotuba rasmi kwa wabunge kuthibitisha kwamba mchakato wa Uingereza kujiondoa EU umeanza.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bi May amewaomba watu walio Uingereza kuungana

Ataahidi "kuwakilisha kila mtu katika Uingereza yote" wakati wa mazungumzo hayo - wakiwemo raia wa EU (wanaoishi Uingereza), ambao bado haijafikiwa uamuzi kuhusu hatima yao baada ya Uingereza kujiondoa kutoka kwa muungano huo.

"Nimejitolea kuhakikisha tunapata mkataba bora zaidi kwa kila mtu katika nchi hii," anatarajiwa kusema.

"Kwani, tunapokabili fursa na changamoto zilizopo mbele yetu, maadili yetu ya pamoja, maslahi na ndoto zetu zinaweza - na ni lazima - zitulete pamoja."


Matukio makuu yanayotarajiwa

  • 29 Machi, 2017 - UIngereza yaanza kutumia Kifungu 50
  • 29 Aprili- Mkutano mkuu wa viongozi 27 wa EU (bila Uingereza) kuipa Tume ya Ulaya ruhusa ya kushauriana na Uingereza
  • Mei - Tume ya Ulaya kuchapisha mwongozo wa mashauriano kwa kufuata ruhusa kutoka kwa viongozi wa EU. EU inaweza kuzungumzia uwezekano wa mashauriano sambamba wa mkataba wa baadaye wa biashara kati ya UK na EU
  • Mei/Juni 2017 - Mashauriano kuanza
  • 23 Aprili na 7 Mei - Uchaguzi wa urais Ufaransa
  • 24 Septemba - Uchaguzi wa ubunge Ujerumani
  • Majira ya kipupwe 2017 - Serikali ya Uingereza inatarajiwa kutunga sheria ya kujiondoa EU na kuweka sheria zote zilizopo chini ya EU kuwa sehemu ya Sheria za Uingereza
  • Oktoba 2018 - Mashauriano yanatarajiwa kukamilika
  • Kati ya Oktoba 2018 na Machi 2019 - Mabunge ya Uingereza, baraza la Ulaya na Bunge la Ulaya kupigia kura mkataba utakaokuwa umeafikiwa
  • Machi 2019 - UK kujiondoa rasmi kutoka EU.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii