Mwanamume amuuma mbwa wa mpenzi wake Puerto Rico

Chihuahua Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Chihuahua, kama huyu aliyepigwa picha Japan, ndiye aliyeshambuliwa na Arroyo

Mwanamume mmoja katika jimbo la Puerto Rico ambalo linamilikiwa na Marekani amefunga jela baada ya kupatikana na hatia ya kumng'ata mwanambwa (kilebu) wa mpenzi wake na kumkata shingo.

Luis Arroyo amefungwa jela miaka saba baada ya kukiri mashtaka ya kumdhulumu mbwa na kumnyanyasa mpenzi wake.

Mwanamume huyo wa miaka 40 alimshambulia mwanambwa huyo aina ya Chihuahua ambaye alikuwa na umri wa miezi miwili katika mji wa Lares magharibi mwa Puerto Rico.

Kadhalika, alimpiga ngumi mpenzi wake tarehe 4 Februari.

Kando na kumfunga jela, Jaji Carlos Lopez Jimenez pia alimpiga Arroyo faini ya $3,000 (£2,400).

Kwa mujibu wa gazeti la El Vocero, Arroyo, ambaye hakuwa na kazi, alikuwa ameishi na mpenzi wake wa miaka 38 nyumba moja kwa miezi sita.

Mwanambwa huyo alifariki papo hapo.

Haijabainika nini kilimfanya mwanamume huyo kumshambulia mbwa huyo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii