Mahakama yaamrisha bunge kutekeleza sheria ya jinsia Kenya

Mahakama yaamrisha kuwepo wanawake zaidi katika bunge la Kenya Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mahakama yaamrisha kuwepo wanawake zaidi katika bunge la Kenya

Mahakama ya juu nchini Kenya imelipa bunge la nchi hiyo siku 60 kutekeleza sheria la usawa wa jinsia la sivyo livunjwe.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya thuluthi mbili ya wabunge waliochaguliwa haisatahili kuwa wa jinsia moja.

Kuna wanawake 69 tu katika bunge la Kenya lenye jumla ya wabunge 349, zikiwemo nafasi 47 zinazotengewa wanawake.

Idadi ya wabunge wanawake itakuwa 117, ikiwa sheria ya thuluthi mbili itatekelezwa.

Lakini bunge limeshutumiwa kwa kushindwa kufunga mwanya huo na mwezi Mei mwaka uliopita bunge lilipiga kura ya kuipinga sheria hiyo.

Mashirika ya kijamii yalipeleka kesi mahakamani kuishinikiza serikali kutekeleza sheria hiyo kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kwa sasa Kenya inachukua nafasi ya 100 kwenye orodha ya nchi 193 katika suala la wabunge wanawake.

Rwanda ndiyo inachukua nafasi ya kwanza ambapo asilimia 61.3 ya wabungi ni wanawake.

Mada zinazohusiana