Gavana wa Mombasa Hassan Joho ahojiwa na polisi Kenya

Bw Joho ni naibu kiongozi wa chama cha ODM Haki miliki ya picha TONY KARUMBA
Image caption Bw Joho ni naibu kiongozi wa chama cha ODM

Gavana wa jimbo la Mombasa katika pwani ya Kenya Hassan Joho ameandikisha taarifa katika afisi za polisi wa kuchunguza jinai katika mji huo kuhusiana na tuhuma kwamba alighushi cheti cha mtihani wa kidato cha nne.

Baraza la Taifa la Mitihani Kenya (KNEC) linadai mwanasiasa huyo wa chama cha upinzani cha ODM alighushi cheti cha mtokeo ya mtihani wa kidato cha nne kumuwezesha kukubaliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi.

Bw Joho, ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha ODM chake waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, amekanusha madai hayo na kudai kwamba serikali imeibua tuhuma hizo ili kumpiga vita.

"Nawaambia kwamba wanachofanya ni kujaribu kuwafanya muamini kwamba sitakuwa kwenye karatasi za wagombea urais lakini nawahakikishia kwamba mradi tu niwe hai, nitakuwa kwenye kura wakati wa uchaguzi Agosti," aliambia wafuasi wake baada ya kuhojiwa na polisi, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation.

Barua ya kaimu afisa mkuu mtendaji wa baraza la mitihani Bi M G Karogo ambayo ilitumwa kwa maafisa wakuu wa uchunguzi wa jinai inaonesha mwanafunzi kwa jina Ali Hassan alifanya mtihani wake katika shule ya upili ya 1993 na akapata alama D- ambayo haiwezeshi mtu kujiunga na chuo kikuu.

Gavana huyo anadaiwa kughushi cheti cha kuonesha alipata alama ya C+ katika mtihani wa mwaka 1992 na akatumia cheti hicho kujiunga na chuo kikuu cha Nairobi ingawa hakumaliza masomo yake.

Bw Joho alijiunga na Chuo Kikuu cha Kampala na akafuzu na shahada katika usimamizi wa biashara mwaka 2013.

Pia ana shahada nyingine ya kwanza kutoka chuo kikuu cha Gretsa cha Kenya.

Nchini Kenya, gavana anahitajika kuwa na angalau shahada ya kwanza kutoka kwa chuo kikuu kinachotambulika nchini Kenya ndipo akubaliwe kuwania wadhifa huo.

Jumanne, Bw Joho aliwaambia wanahabari kwamba anajivunia alama ya mtihani ya D- ambayo alipata katika mtihani wa kitaifa wa mwaka 1993.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii