Waziri wa Marekani Rex Tillerson kuzuru Uturuki

Rex Tillerson Haki miliki ya picha AFP / Getty Images
Image caption Bw Rex Tillerson atakutana na Rais Erdogan

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson atazuru Uturuki leo huku uhusiano kati ya washirika hao wawili wa shirika la kujihami la nchi za Magharibi, NATO, ukidorora.

Atakutana na Rais Erdogan na maafisa wengine wa ngazi ya juu kwa mazungumzo yatakayolenga vita dhidi ya kundi la Islamic State katika nchi jirani za Syria na Iraq.

Huu ni mkutano wa kiwango cha juu zaidi kati ya maafisa wa Uturuki na Marekani tangu Donald Tump aingie madarakani.

Tofauti zinaongezeka kimsingi kutokana na nani anapaswa kuhusika katika kuudhibiti upya mji wa Syria wa Raqqa kutoka kwa kundi la Islamic State.

Uturuki inataka Marekani isitishe muungano wake na wapiganaji wa Kikurdi lakini Washington inasema ndicho kikosi kizito chenye uwezo huo.

Rex Tillerson leo atalijadili suala hilo licha ya kuwa kuna ishara ndogo kuwa Marekani itabadili msimamo wake.

Serikali ya Uturuki pia itamshinikiza Bw Tillerson kuhusu ombi lake la kumhamisha Fethullah Gulen, kiongozi wa kidini anayeishi Pennsylvania ambaye serikali ya Ankara inamtuhumu kwa jaribio la mapinduzi.

Hatahivyo mashirika ya kijasusi ya Ulaya yametilia shaka tuhuma hizi.

Marekani inasisitiza linapaswa kusalia kuwa uamuzi wa kisheria kuliko wa kisiasa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii